Tanzania ina warembo wengi. Walimbwende kwelikweli. Masupastaa wengi wa kike lakini kuna namna wote wanasalimu amri kwa Wema Isack Sepetu.
Sio leo, lakini juzi jana na hata kesho Wema Sepetu bado ana nafasi kubwa ya kuendelea kuwaburuza tu na hiyo ni kutokana na namna alivyojiweka tangu akiwa mdogo, binti na sasa wakati ambao umri umesogea.
Wema amefanya mambo mengi, mabaya na mazuri lakini nyota yake kwenye tasnia ya ulimbwende na sanaa haijawahi kushuka kamwe. Utapigwa mawe ukitaja mastaa wa kike wa muda wote nchini bila kutaja jina lake.
Mwanaspoti kupitia makala haya linakuletea uchambuzi wa ‘usupastaa’ wake kuanzia mwanzo wake hadi sasa. Tiririka.
WAKISHUA Moja ya vitu vya tofauti kwa Wema na mastaa wengine wa kike nchini ni kuwa ‘yeye ni wa kishua’.
Wema ni binti pendwa wa aliyekuwa mwanadiplomasia mahiri nchini, Abraham Sepetu ambaye aliwahi kuwa waziri katika Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar sambamba na Tanzania bara kwa nyakati tofauti.
Unaambiwa Wema alikuwa kipenzi cha baba hivyo alipewa maisha yote ya kishua aliyoyataka kuanzia nyumbani hadi shuleni na kote alikuwa hashikiki.
Shule alisoma Academic International, moja ya shule za kishua wakati huo na alikuwa miongoni mwa wanafunzi wachache waliokuwa wakipelekwa na kufuatwa kwa ndinga binafsi huku wengine wakipanda mabasi ya shule ila yeye alikaa siti ya mbele ya gari binafsi. Utamuambia nini?
Baada ya hapo alienda Malaysia kusoma Chuo na wakati huo tayari alikuwa ametwaa tuzo ya Miss Tanzania aliyoichukua mwaka 2006 akiwa kidato cha sita. Hii ndio ile Waswahili husema “mwenye nacho huongezewa.”
Wema ameendelea kuishi maisha ya kishua hadi leo. Anasukuma ndinga kali, masikani pamepoa lakini pia haumuoni hadi ulipie. Ni adimu sana.
MISS TANZANIA Hapa ndipo Wema amechora mstari na mastaa wengine wa kike hapa Bongo kwani mwaka 2006, ulizalisha masupastaa wengi kupitia shindano la ‘Miss Tanzania’ chini ya Hashimu Ludenga, wakali unaowaona sasa, baadhi yao walipita kwenye chujio hilo lakini mwisho wa siku ndiye aliibuka mshindi.
Wema wakati huo aliwabwaga ‘masistaduu’ kibao wakiwemo, Jokate Mwegelo kwa sasa ni muheshimiwa, Lisa Jensen, Irene Uwoya na Anti Ezekiel, mchuano ulikuwa mkali lakini akashinda ila leo kwa sasa wote ni mastaa hapa nchini.
Wema huenda akawa Miss Tanzania maarufu zaidi kuwahi kutokea. Anatisha sana kwani tangu alipotangazwa mwaka 2006 akichukua kijiti cha Nancy Sumari ambaye pia alifanya makubwa kwenye tasnia hiyo hakuna aliyekanyaga levo zake kwa umaarufu.
Baada ya Wema, wamechaguliwa mamiss Tanzania 15 lakini hakuna hata mmoja aliyefikia umaarufu wake, achana na mafanikio, elewa neno ‘umaarufu’. Huenda hata wengine ukawa hauwajui, ngoja nikutajie hapa kuanzia mwaka 2007 hadi sasa labda utaokotaokota baadhi ya majina.
Richa Adhia, Nasreen Karim, Miriam Gerald, Genevieve Mpangala, Salha Kifai, Lisa Jensen, Brigitte Lyimo, Happiness Watimanywa, Lilian Kamazima, Diana Edward Lukumai, Julitha Kabete, Queen Elizabeth Makune, Sylvia Sebastian, Juliana Rugumisa, Halima Kopwe na Tracy Nabukeera wa mwaka 2024. Umemkumbuka nani? Tuishie hapa ila kiufupi Wema ni wa moto, juzi, jana na leo.
BONGO MUVI Huku pia Wema hashikiki na amefanya makubwa kinoma tangu pale alipoanza kuonekana kwenye tambala lililoitwa ‘A Point of No Return’ ambapo alikuwa muhusika mkuu akitumia jina la ‘Dina’ sambamba na marehemu, Steven Kanumba aliyetumia jina la ‘Lameck’ na baada ya hapo kilichofuata ni historia.
Nakudokeza tu wakati huu wawili hao walikuwa kwenye penzi nzito. Baada ya hapo Wema ameonekana kwenye zaidi ya filamu 30, ambapo nyingi amekuwa mhusika mkuu chini ya waandaaji tofauti.
Family Tears, Red Valentine, Sakata, Tafrani, White Maria, The Diary, 14 Days, House Boy, Basilisa, DJ Ben na Crazy Tenant ni baadhi ya filamu ambazo alicheza.
Siku nikikutana naye nitamuuliza lini ile sinema iliyotambulishwa pale Kilimanjaro Hyatt Regancy, mwaka 2012 ikiitwa ‘Superstar’ aliyocheza na Diamond Platnumz wakati wako penzini itatoka lini? Nitawajibu akinijibu.
Hadi sasa Wema ni miongoni mwa waigizaji bora wa kike lakini yupo meza moja na waigizaji wa kike ambao ukiwahitaji kwenye kazi yako lazima uvunje benki, umlipe mkwanja mrefu.
Aidha, Wema amecheza filamu kibao, pia amechukua tuzo mbalimbali ndani na nje kupita sanaa hii.
UKIMDATE UMETOBOA Achana na madoni waliodaiwa kuwahi kutoka kimapenzi na Wema, hapa unasimuliwa baadhi ya wanaume waliokuwa wamepoa na moja kwa moja supastaa huyo akakoleza na kuwabusti kwenye kazi zao na hadi sasa wametoboa kinoma noma.
Unaanza na Kanumba ambaye licha ya kujipata tayari lakini kuwa penzini na Wema kuliongeza baadhi ya pointi kwenye ustaa wake.
Baada ya hapo walifuata wengine akiwemo mshindi wa ‘Big Brother’ Idriss Sultan ambaye ilizuka skendo ya Wema kumfilisi lakini hata hivyo mchekeshaji huyo alijizolea umaarufu zaidi kupita penzi lake na Wema lililokufa mwaka 2016.
Wengine ambao inasemekana waliwahi kupenzika naye ni mwanamitindo Calisah, wanamuziki Mr Blue, TID, Chaz Baba na Ommy Dimpoz ambao wote kila mmoja kwa wakati wake alinufaika na ustaa wa nyota huyo licha ya kwamba taarifa hizi sio rasmi.
Uhusiano wa Wema ambao ulitrend zaidi ni pale alipokuwa akitoka kimapenzi na staa wa Bongo Fleva, Diamond Platinumz.
Ilikuwa kati ya 2012-2014 ambapo wawili hao walikuwa kwenye huba zito hadi kufika kuvishana pete ya uchumba lakini hata hivyo mapenzi yao hayakudumu na baadaye kila mmoja kushika hamsini zake baada ya kutumiana.
Kwa sasa Wema yuko penzini na mwanamuziki Whozu na penzi lao liko moto huku wakipachikana majina ya ‘Chimama’ kwa Wema na ‘Chibaba’ kwa Whozu, kiufupi hauwaaambi kitu wawili hao kwa sasa.
KOTE YUPO Wema yupo kote kote. Watu wake wa karibu sana wanamzungumzia kama mtu mwenye tabia nyingi kuna muda anakuwa mpole na nyakati nyingine huwa mkali pia ni mtu wa watu na wala haringi kama wengi wanavyodhani.
Wema utamkuta kwenye siasa, utamkuta katika shughuli za kijamii. Kwenye muziki, muvi, mitindo na mitandao huko kote yupo na anakaa siti za mbele kabisa.
Kwa nyakati tofauti amebadili muonekano wake, kuna muda alikuwa mwembamba, wakati mwingine akawa mwenye umbo lililonona na sasa amerejea kwenye wembamba. Kote yupo na amepita na huyo ndiye Wema Sepetu anayebeba jina la nchi la ‘Tanzanian Sweetheart’.
Kwa sasa Wema anaendelea na kazi zake za sanaa ikiwemo uigizaji na uzalishaji filamu na tamthilia pia kazi za utangazaji na bado ni wa moto akiwa miongoni mwa Watanzania wanawake wenye ushawishi zaidi nchini. Kule Instagram ana wafuasi milioni 11.3.