Yanga Acheni Kujidanganya, Kushinda Dhidi ya Mamelod Kunahitaji Mikakati ya Kikubwa

 

Yanga Acheni Kujidanganya, Kushinda Dhidi ya Mamelod Kunahitaji Mikakati ya Kikubwa

Ni timu chache sana duniani zenye kikosi kipana. Mara nyingi sana timu ikishajipata huwa inadhani ina kikosi kipana.


Yanga ndiyo timu bora nchini kwa sasa. Hili halina ubishi wowote. Lakini hawana kikosi kipana. Kuwa na kikosi kipana maana yake ni kuwa na wachezaji ambao yeyote anayepangwa timu inashinda.


Ni kuwa na wachezaji walau wawili kwenye kila nafasi ambao hawatofautiani sana kwenye ubora.


Kuna mtu unaona anakaribia uwezo wa Djigui Diarra pale? Kwenye orodha ya makipa pale Yanga, unamwona yetote anayesogelea kiwango chake? Jibu ni hapana.


Hakuna kikosi kipana pale Jangwani. Kuna kikosi cha kwanza bora kuliko timu zote nchini kwa sasa.


Yanga iliwahi kufanya mabadiliko makubwa sana ya wachezaji msimu huu chini ya Kocha Gamondi dhidi ya Ihefu FC, Mbarali, Mbeya na kilichotokea wote tunajua. Yanga alifungwa vizuri tu.


Yanga alifanya pia mabadiliko makubwa ya wachezaji kwenye mechi ya ugenini dhidi ya Kagera Sugar, Chupu Chupu! Akaambulia Sare.


Nimetazama mechi ya juzi dhidi ya Azam FC, kupoteza wachezaji wake muhimu kwa majeraha kuliwaumiza sana Wananchi. Yanga wana kikosi bora, sio kikosi kipana.


Akikosekana Khalid Aucho, unaona kabisa mashimo mengi uwanjani. Pamoja na kuwa Aucho yuko maji ya jioni lakini hakuna wa kuziba pengo lake. Hakuna kikosi kipana pale. Gamondi katengeneza kikosi bora. Wanaokuja kutoka benchi, wengi ni wa kawaida na sasa kachangia kocha wao.


Tofauti nyingine kubwa kati ya Gamondi na Nabi, ni kuusoma mchezo na kufanya maamuzi magumu. Wakati Yanga iko na Nabi, ilikuwa hatari sana akifanya mabadiliko ya wachezaji.


Huyu wa sasa katengeneza kikosi chake cha kwanza tu. Akibadilika kidogo tu timu inapoteza ubora. Watu kama Farid Mussa, Kibwana Shomary, Augustine Okrah walipaswa kupewa muda wa kutosha uwanjani ili linapotokea lolote waisaidie timu.


Gamondi ana kikosi chembamba sana. Anabebwa tu na ubora wa mchezaji mmoja mmoja. Kunahitajika mzunguko wa wachezaji wengi sana kupewa nafasi ili wawe na utayari pale wanapohitajika.


Kocha ni kama amekariri kikosi chake. Hataki kubadilika. Hataki kutoa nafasi kwa wachezaji wengi zaidi.


Suala la kuwa na kikosi kipana, sio jambo la kitoto. Yanga akiumia tu Pacome Zouzoua watu wanashikwa na tumbo la uzazi.


Gamondi ana wachezaji wengi lakini amewatumia wachache. Ameshindwa kutengeneza mzunguko mzuri wa wachezaji wake. Wachezaji wanaombeba ni wale wale. Kikosi chake cha kwanza kinatabirika. Anaweza kuwa na wakati mgumu sana akienda msimu wa pili.


Amekuwa na tabia ya kuchelewa kuusoma mchezo na kufanya mabadiliko.


Yeye akishapata kikosi chake cha kwanza, shughuli imeisha! Mengine yanayofuata ni kupiga ramli chonganishi!


Gamondi ana mtihani mkubwa mbele yake.


Amejipatia heshima kubwa sana kuipeleka Yanga robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika. Nasreddine Nabi alishindwa. Lakini Yanga wana tamani kufika mbali zaidi msimu huu.


Kama Gamondi asipojipanga vizuri, Yanga wanaweza kupoteza mechi tatu mfululizo. Tayari wamefungwa na Azam FC na mbele yao wana mechi mbili mfululizo dhidi ya moja ya timu bora Afrika, Mamelod Sundowns.


Kukosekana kwa Pacome, Yao Yao na Aucho kunaacha pengo kubwa. Yanga haiwezi kuwa salama bila hao watu. Gamondi ana kikosi chembamba sana. Hapa ni kumwombea Pacome na Yao walau wauwahi mchezo huu wa kwanza.


Yanga anahitaji kushinda mechi ya kwanza bila kuruhusu bao lolote nyumbani. Kwenye hatua za mtoano na hasa kwa kanuni zetu za bao ugenini, ni vyema kushinda hata bao moja tu lakini usiruhusu nyavu zako kuguswa.


Gamondi inabidi achangamke. Akipoteza mechi tatu mfululizo hali haitokuwa shwari Jangwani.


Mechi ya kwanza nyumbani ni muhimu sana kushinda ili kuweka mipango ya kusonga mbele hai.


Chini ya Gamondi tatizo ni kukosa tu mzunguko sawia wa wachezaji.


Ametumia wachezaji wale wale karibu kila mechi. Na kwa sababu hajawaandaa wengi ndiyo maana wakianza tu unaona utofauti mkubwa.


Alipaswa kama kocha kutengeneza balansi nzuri kati ya wachezaji chaguo la kwanza na wale chaguo la pili. Ili wote wawe bora ni lazima wapate muda wa kucheza. Hakuna mchezaji yeyote anayeimarika akitokea benchi.


Mamelodi ndiyo mtihani namba mbili baada ya Azam FC. Kama una siku nyingi hujawaona, ni wale wale waliounda kikosi cha Bafana Bafana kwenye fainali za Mataifa ya Afrika zilizomalizika hivi karibuni Ivory Coast.


Wachezaji karibu saba wa Mamelodi walikuwa kwenye kikosi cha kwanza cha Bafana Bafana.


Sio timu ya kubeza. Inahitajika mipango madhubuti kuwafunga. Sio timu ya kutisha sana lakini sio timu nyepesi.


Ni timu ya kizazi kipya yenye uwekezaji mkubwa. Ni timu ya kizazi kipya iliyofanikiwa kumaliza ufalme wa Orlando Pirates na Kazier Chiefs pale kwa Mzee Madiba.


Wamejipanga sawa. Gamondi anahitaji kuwa na wanajeshi wake kamili kwenye vita hii ya Ligi ya Mabingwa Afrika.


Gamondi anatakiwa kuchangamka. Mambo ya kulalamikia waamuzi hayasaidii zama hizi. Kufungwa ni kufungwa tu. Mechi ya Azam inapaswa kuchukuliwa kwa uzito mkubwa mno.


Makosa yaliyotokea yanapaswa kufanyiwa kazi. Mamelodi ni zaidi ya Azam FC mara 10. Gamondi na vijana wake ni lazima wajipange sawa sawa.


Ndiyo maana kauli za kusema Yanga ina kikosi kipana, sijawahi kuzielewa. Yanga ina wachezaji wa kikosi cha kwanza tu walio bora. Ukifanya mabadiliko madogo tu timu inapoteza uelekeo.


Uchezaji pia unakuwa ni tofauti sana. Anayeweza kubadilisha upepo huu ni Gamondi. Lakini bado Yanga inategemea ubora wa wachezaji wale wale wa kikosi kinachoanza na hakuna mbadala wenye kuleta muujiza.


Kushinda dhidi ya Mamelodi kunahitaji mikakati ya kikubwa. Kila la heri Wananchi, ni muhimu sana kushinda mechi ya nyumbani bila kuruhusu bao.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad