Yanga: Hao Mamelodi Faili Lao Tunalo, Kocha Mwingereza Aongeza mbinu

 

Yanga: Hao Mamelodi Faili Lao Tunalo, Kocha Mwingereza Aongeza mbinu

Mabosi wa Yanga tangu walipofahamu timu hiyo itavaana na Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini katika mechi za robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika hawalali. Wamekuwa wakipambana kunasa kila taarifa muhimu inayowahusu wapinzani hao ili kuwapa kazi nyepesi Machi 30 watakapokutana kwa mechi ya kwanza na Aprili 5 watakaporudiana.


Yanga imeamua kumtumia Mpho Maruping ambaye ndiye mchambuzi wa mikanda ya mechi za wapinzani (video analyst) kupata kila taarifa za ufundi ili kukamilisha kazi ya kuijua Mamelodi kabla ya timu hizo kukutana Machi 30 Kwa Mkapa.


Lakini wakati wamefanikiwa kudukua faili la Mamelodi, ghafla wakapata zali kutoka kwa kocha Mwingereza anayefundisha soka huko Afrika Kusini kwa kuwapa mbinu mpya za kuweza kuimaliza wababe hao wa Sauzi kitu ambacho ni kama kinamrahisishia kazi Kocha Miguel Gamondi.


Ipo hivi. Yanga inajua mashushushu wa Mamelodi Sundowns walikuwapo Dar es Salaam kuifuatilia timu hiyo ili kujua ubora wa uwanjani na wamemaliza kazi na kurudi kwao kisha wakashushwa wengine ambao wanafuatilia mambo mengi ya nje ya uwanja lakini nao wamejibu mapigo kibabe wakisema hata wao wanajua kila kitu kuhusu wao baada ya kudukua faili zima kupitia Msauzi mwenzao.


Salamu ambazo Yanga imezitupa kwa Mamelodi ni kuwaambia kwamba kila kitu kuhusu ufundi wao wa uwanjani upo chini ya kocha Miguel Gamondi baada ya fundi mmoja wa Kisauzi kumaliza kazi yake akitumia wiki moja tu kufanya umafia mzito.


Yanga imemtumia Mpho Maruping ambaye ndiye mchambuzi wa mikanda ya mechi za wapinzani (Video Analyst) kupata kila taarifa za ufundi kukamilisha kazi ya kuwajua Mamelodi kabla ya timu hizo kukutana saa 3:00 usiku ya Machi 30 pale Kwa Mkapa.


Maruping ambaye faida kubwa kwa Yanga ni kwamba ameucheza mpira akiwa mwanasoka mstaafu ameshakabidhi mikanda ya kutosha ya Mamelodi wakiwa ndani ya msimu huu.


Ingawa, Yanga inafanya siri kubwa kuweka wazi juu ya taarifa hizo za kiufundi wapinzani wao wakiwa chini ya kocha kijana fundi Rhulani Mokwena, lakini taarifa za mifumo yote tayari ipo kwa Gamondi ambaye naye amethibitisha kupata anachokitaka.


“Sisi hatujalala tupo kazini hasa na sasa tuna kila kitu kuhusu Mamelodi tumeamua kwenda kupambana nao kimyakimya, kila kitu kuhusu ufundi wao wakiwa ugenini makocha wetu washavipata tena muda mrefu,” alisema bosi huyo wa juu wa Yanga na kuongeza:


“Bahati kubwa kwetu ni kwamba tuna benchi la ufundi ambalo mbali na kuijua Mamelodi pia tumefanikisha kupata kila taarifa zao kirahisi ambazo makocha wameridhika kwamba wamepata mambo muhimu.


“Tunachokiomba tu ni wachezaji wetu kurejea salama kwenye majukumu ya timu za taifa, tumeacha wao waseme mitandaoni, hatujatoka mchezoni na watu wanavyoichukulia hii mechi, tunawaheshimu Mamelodi lakini dakika 90 za nyumbani zitatuheshimisha tena.”


“Tunajua pia hadi wachezaji wanaotakiwa wanabanwa na kutocheza kwa uhuru uwanjani ambao ndio injini ya timu yao kuamua mechi, hivyo ukiongeza na ufundi wa kocha ambaye anawajua kwa undani tumetulia,” aliongeza kigogo huyo.


Hesabu kubwa kwa Yanga sasa ni kuhakikisha kiungo wao Khalid Aucho anafuzu vipimo vya uponaji na kuwa tayari kwa mchezo huo baada ya mwenyewe kujifua vikali akiitaka mechi hiyo.


KOCHA MWINGEREZA


Kocha Mwingereza aliyewahi kuinoa Simba kwa mafanikio japo kipindi kifupi, Dylan Kerr amekiongezea kikosi cha Gamondi mbinu mpya kwa kuwaambia kwamba ili wawanyooshe ni lazima watumie mfumu wa kushambulia kwa ghafla (counter Attack).


Kerr aliyefundisha akiwa Afrika Kusini kwa miaka zaidi ya sita kupitia timu za Moroka Swallows FC, Tshakhuma, Black Leopards FC na Baroka FC, amefichua ameshakabiliana na Mamelodi kwa zaidi ya mara nne na kwamba anajua udhaifu wao upoje ikiwa chini ya Rhulani Mokwena.


Kocha huyo ambaye kwa sasa yupo Uingereza kwa mapumziko aliliambia Mwanaspoti kuwa, ni muhimu kwa Gamondi kuiandaa timu kucheza kwa kushambulia kwa kasi hasa wanapovuka mstari wa kati huku wakizuia Mamelodi kwa nidhamu ya hali ya juu.


Kerr alisema ubora wa Mamelodi upo katika eneo lake la kiungo na ndio maana wamekuwa na uwezo mkubwa wa kumiliki mpira, ikiwa pia ni timu iliyoongozwa kwa kumiliki mchezo katika mechi za makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa msimu huu kulinganisha na timu nyingine 15 ikiwamo Yanga.


“Naijua vizuri Mamelodi Sundowns, ni timu nzuri na bora yenye uwezo mkubwa wa kumiliki mpira, udhaifu wao nimekuwa nikiuona wakati wakishambulia maana huwa na namba kubwa ya wachezaji wanaosogea kwenye eneo la wapinzani, hivyo kama wapinzani ana wachezaji wenye kasi ni rahisi kufungika,” alisema Kerr na kuongeza;


“Nakumbuka wakati nikiwa na Baroka tuliwafunga bao 1-0, baada ya hapo tulifunga njia zote, kila ambapo walisogea kwenye eneo letu tuliwanyima uhuru wa kumiliki mpira hadi mchezo unamalizika tulifanikisha kile ambacho tulikilenga.


“Yanga wanatakiwa kuwa makini, wanatakiwa kuwa kwenye kiwango chao kama ilivyokuwa dhidi ya Simba na kwa bahati nzuri nimewaona wana wachezaji wanaoweza kuwa na madhara kwa Mamelodi kikubwa ni kucheza kitimu na nidhamu na jukumu la kuzuia liwe la kila mchezaji katika nafasi yake.”


Mamelodi inawategemea zaidi viungo wake, Teboho Makoena, Lebohang Maboe, Marcelo Iván Allende, Themba Zwane, Thembinkosi ‘Nyoso’ Lorch na Lucas Costa wanaomlisha Peter Shalulile.


Kerr katika kikosi cha Yanga ameeleza kuvutiwa na uwezo wa Stephane Aziz Ki, Pacome Zouzoua na Mudathir Yahya kwa kusema wanaweza kuwa mwiba kwenye mchezo huo, lakini upande wa Mamelodi alimtaja Mbrazil, Lucas Costa na Peter Shalulile ambao wamechangia zaidi ya nusu ya mabao (33) waliyonayo kwenye ligi.


Costa ndiye kinara wa mabao kwenye ligi ya Afrika Kusini akiwa na mabao 10 na asisti mbili, Shalulile ana mabao manne na asisti mbili, jumla nyota hao wamehusika kwenye mabao 18. Kwa upande wa Yanga, Aziz ana mabao 13, Mudathir (8) huku Pacome akiwa na saba, wachezaji hao ambao wametajwa na Kerr kwa pamoja wamefunga mabao 28 kati ya 49 iliyonayo Yanga kwenye ligi.


Rekodi zinaonyesha Mamelodi iliyomaliza kinara wa kundi A ikiwa na pointi 13 imetumia mifumo ya 4-4-1-1 ikiishinda TP Mazembe kwa bao 1-0 nyumbani, lakini ikaenda kupoteza ugenini pia kwa bao 1-0 baada ya wapinzani wao kutumia mbinu za kushambulia kwa kushtukiza na kujilinda kwa nidhamu.


Ikashinda mechi ya pili ugenini dhidi ya Pyramids kwa ushindi kama huo ikitumia mfumo wa 3-4-3 ikibadilika na kuwabana Waarabu hao.


Mchezo mwingine wa ugenini kushinda ni dhidi ya Nouadhibou kwa ushindi wa mabao 2-0 ukiwa ndio ushindi mkubwa ugenini Mokwena akibadilika tena akitumia mfumo wa 4-3-3.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad