Yanga Vs Mamelodi... Vita ya Dakika 90 kwa Mkapa

Yanga Vs Mamelodi... Vita ya Dakika 90 kwa Mkapa


Dakika 90 katika uwanja wake wa nyumbani wa Benjamin Mkapa dhidi ya Mamelodi Sundowns leo kuanzia saa 3:00 usiku zimeshikilia kwa kiasi kikubwa fursa ya Yanga kuandika historia ya kucheza hatua ya nusu fainali na hata fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika.


Ushindi katika mechi hiyo ya leo, utarahisisha kazi Yanga katika mechi ya marudiano itakayochezwa Afrika Kusini mwishoni mwa wiki ijayo ambapo utaifanya ihitaji sare tu au ushindi wa aina yoyote ugenini ili itinge hatua ya nusu fainali.


Yanga inaikabili Mamelodi ikitegemea zaidi makali ya safu yake ya ushambuliaji ambayo imeonekana kuwa tishio katika hatua ya makundi ingawa wasiwasi upo katika safu ya ulinzi iliyoonyesha kusuasua kwenye hatua iliyopita.


Katika mechi sita za hatua ya makundi ya mashindano hayo, Yanga imepachika mabao tisa ikiwa ni wastani wa bao 1.5 kwa mchezo na haikupata bao katika mechi mbili tu huku safu yake ya ulinzi ikifanya vibaya kwa kuruhusu mabao sita sawa na wastani wa bao moja kwa kila mchezo.


Mamelodi inaonekana kuwa na takwimu bora, zaidi kwenye eneo la ulinzi ikiwa kwenye michezo ya hatua ya makundi imeruhusu bao moja pekee, lakini safu yake ya ushambuliaji ikifunga sita sawa na wastani wa bao moja kwenye kila mchezo ambao ilicheza.


Takwimu bora ambazo Mamelodi Sundowns wamekuwa nazo katika mashindano ya kimataifa pindi wanapokuwa nyumbani, zinawalazimisha wachezaji wa Yanga kuhakikisha wanapambana kuibuka na ushindi leo.


Kuna zaidi siku 1082, ambazo timu hiyo haijapoteza mechi yoyote ya Ligi ya Mabingwa Afrika ambayo ilikuwa mwenyeji nchini Afrika Kusini.


Tangu ilipofungwa mabao 2-0 nyumbani na CR Belouizdad, Aprili 9, 2021, Mamelodi haijapoteza tena mchezo wa mashindano hayo ikiwa Afrika Kusini ambapo katika mechi 16 zilizofuata, imeibuka na ushindi mara 12, ikitoka sare nne.


Mchezo huo utachezeshwa na marefa wote sita kutoka Misri ambapo wa kati atakuwa ni Amin Mohamed akisaidiwa na Mahmoud Ahmed na Ahmed Hossam huku kwenye chumba cha teknoklojia ya video ya usaidizi kwa marefa wakiwepo Mahmoud Ashor na Mahmoud Elbana.


Refa Amin anakumbukwa na wengi nchini kwani ndiye alichezesha mechi ya mwisho ya hatua ya makundi ya Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon) 2023 baina ya timu ya taifa ya Tanzania 'Taifa Stars' na ile ya DR Congo ambayo ilimalizika kwa sare tasa.


NOTI NJE NJE


Achana na fedha ambazo nyota wa Yanga watavuna kutoka klabuni kwao ikiwa itaibuka na ushindi leo, kuna uhakika wa zaidi ya Shilingi 3 bilioni ikiwa itafanikiwa kuitupa nje Mamelodi Sundowns na kutinga nusu fainali.


Ikiwa itatinga nusu fainali, Yanga itajihakikishia kiasi cha Dola 1.2 milioni (Sh3 bilioni) ambazo ni fedha zitolewazo na Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) kwa kila timu ambayo itakomea katika hatua hiyo.


Kocha Miguel Gamondi wa Yanga na Rulani Mokwena kila mmoja ametamba kuwa timu yake itaonyesha kandanda la kuvutia na itajitahidi kupata matokeo mazuri kwenye mechi hiyo.


"Tunataka kufanya vizuri katika hatua ya mtoano, hiyo itatupa tathmini nzuri ya wapi tulipofikia. Tutajitahidi kufanya kila liwezekanalo tupate matokeo mazuri ambayo ni muhimu. Ni mechi ngumu hasa kwetu lakini tutajitahidi kuhakikisha tunafanya vizuri," alisema Gamondi.


Kocha Mokwena wa Mamelodi Sundowns alisema,"Kwangu sijawahi kuutazama mchezo wa mpira wa miguu kwenye kujilinda zaidi (kupark bus) bali nautazama mpira wa miguu kama burudani ambayo inapaswa kuambatana na matokeo mazuri.


"Hakuna kitakachobadilika dhidi ya Yanga, kuhusu mbinu ni siri yangu na wachezaji wangu, naamini tuna kaka na dada wengi tu hapa Tanzania ambao watakuja kutushangilia.”

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad