Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Klabu ya Simba, Ahmed Ally amesema kuwa timu hiyo inapitia wakati mgumu ndani ya wiki mbili baada ya kupata matokeo mabovu na kuondoshwa kwenye baadhi ya michuano lakini haiwafanyi mashabiki wa timu hiyo kuwa wanyonge.
Ahmed amesema hayo jana baada kurejea Dar wakitokea Singida kwenye mchezo wa Ligi ambao Simba ilitoa sare huku ikiwa na kibarua kingine Aprili 20, mbele ya watani zao, Yanga SC.
“Tumekuwa na wiki mbili ngumu tukipitia matokeo mabaya kwenye mechi tatu, ni sehemu ya maisha ya mpira wa miguu. Kuna wakati unashinda na kuna wakati unapoteza lakini hatuna namna zaidi ya kuyapokea matokeo na kupambana ili tufanye vizuri kwenye mechi zijazo.
“Hakuna haja ya kutupiana lawama, haiwezi kutusaidia badala yake tuungane. Tumeondolewa CFCL, tumeondolewa Kombe la Shirikisho na tumepoteza mbele ya Ihefu lakini hii haitupi nafasi ya kukata tamaa, tunaamini nafasi ya kupata ubingwa wa ligi bado tunayo.
“Malengo yetu sasa ni mechi ya Jumamosi dhidi ya Yanga, ni mechi inayobeba taswira ya soka la Tanzania ambao unabeba heshima ya Tanzania na sisi kama Simba tunayo nafasi ya kwenda kuweka heshima yetu kwenye mchezo wa dabi. Ni lazima tuhakikishe tunaingia vizuri na kushinda.
“Tulipoteza duru ya kwanza, hatupo tayari kuona tunapoteza tena kwa mara ya pili kwenye msimu mmoja. Niwaombe Wanasimba ambao wamekata tamaa, mioyo inavuja damu, waje uwanjani kuipigania Simba na kurejesha heshima yetu, tukishikamana hakuna wa kutuzidi nguvu, ajenda yetu ni kwenda kumfunga mtani," amesema Ahmed Ally.