Klabu ya Simba imesema kuwa aliyekuwa kocha wao, Abdelhak Benchikha aliomba tangu mapema kuwa aachane na timu hiyo ili aende nyumbani kwao nchini Algeria kwa ajili ya kumuuguza mkewe lakini uongozi wa Simba ulifanya jitihada za kumbakisha licha ya jitihada hizo kugonga mwamba.
Hayo yamesemwa na Meneja Habari wa Simba, Ahmed Ally wakati akizungumza kuhusu kuondoka kwa kocha huyo aliyejiunga na Wanalunyasi mwishoni mwa msimu uliopita akichukua nafasi ya Robertinho aliyefungashwa virago.
“Tumetangaza kuachana na kocha Benchikha na taarifa imewafikia Wanasimba kote duniani, ni taarifa ambayo imewaumiza sio mashabiki tu tu hata uongozi wa Simba umeumia sana kwa sababu ya ukubwa wake na CV yake tulitamani kuendelea kuwa naye ili kuisaidia Simba kufikia malengo yetu. Tuliamini kwa uwezo, uzoefu na ubora wake lilikuwa chaguo sahihi kwetu, tulitamani kuwa naye kwa muda mrefu ili project yetu itimie.
“Mwalimu Benchikha alihitaji kuondoka mapema, baada ya mechi ya Al Ahly tu alitoa taarifa kuwa anataka kuondoka, juhudi za viongozi kumbakisha zilizonga mwamba. Viongozi waliomba angalau amalizie msimu lakini hakuwa tayari akasisitiza kuwa huu ni muda wake muafaka kuondoka. Alisema anauguliwa na mkewe na ni maradhi makubwa hivyo anahitaji kuwa karibu na mkewe kumuuguza.
“Alisema kwa sasa akili yake haipo kabisa kwenye kazi, akili yake inawaza jambo lake hilo la kifamilia, hata kama ataendelea kubaki, badi kuna uwezekano wa kuharibu kazi, hivyo ili asiharibu kazi ni vyema akaiacha Simba akaenda kushughulika na jambo lake, viongozi tuliamua kumruhusu aondoke. Duniani kote mwalimu kuondoka huna namna ya kumzuia. Benchikha ameshaondoka na sasa tunalazimika kuongia kwenye mchakato wa kutafuta kocha mwingine.
“Kocha ameondoka kwa sababu zake binafsi sisi hatuwezi kumzuia. Niwatoe hofu Wanasimba, kama tuliweza kumleta kocha Benchikha ambaye ni namba mbili Afrika kwa ubora, hatushindwi kumleta kocha yoyote yule ambaye tutaona anafaa kuisaidia Simba. Fedha tunayo, jicho la kuangalia kocha mzuri tunalo, tunakwenda kuendelea tulipoishia, viongozi wapo kazini kuangalia mwalimu atakayetufaa kuifundisha Simba yetu na kuisaidia kupata mafanikio," amesema Ahmed.
Kwa sasa Simba inanolewa na kocha wa muda, Juma Mgunda akisaidiana na Suleimani Matola katika kipindi cha mpito mpaka mwisho wa msimu wakati uongozi wa klabu ukitafuta kocha mwingine.