Aziz Ki Apigia Saluti Asisti ya Aucho iliyoiua Simba

Aziz Ki Apigia Saluti Asisti ya Aucho iliyoiua Simba

 

Staa wa Yanga, Stephane Aziz Ki, ambaye amekuwa maarufu kwa pasi zake za hatari za kuchana ukuta wa upinzani, amempigia saluti Khalid Aucho kwa pasi iliyoizamisha Simba katika ushindi wa 2-1 wa timu ya Wananchi katika Kariakoo Dabi Episode 3 juzi.


Aucho alipiga pasi ya kiwango cha dunia iliyopita juu ya ukuta wa Simba ambayo straika Joseph 'Guedowski' Guede aliikontroo hewani kwa ufundi wa hali ya juu baada ya kuukwepa mtego wa kuotea kabla hajampiga chenga kipa wa Simba, Ayoub Lakred na kumwacha amelala chini akifunga bao katika lango tupu.


Baada ya admini wa ukurasa wa Instagram ya Yanga akiposti video ya bao hilo huku akimmwagia maua yake mfungaji wa bao hilo, Guede kwa kumwita 'Guedowski', Aziz Ki aliona zaidi ya bao na mfungaji katika upatikanaji wa bao hilo.


Aziz aliona kitu kikubwa katika pasi ile ya kiwango cha SGR kutoka kwa Aucho na hakuacha kumshukuru kiungo huyo wa ulinzi raia wa Uganda.


"Asante kwa ile pasi @auchokhalidofficial wewe ni wa kipekee," aliandika Aziz katika mnyororo wa comments za posti hiyo.


Aucho aliyaona maua yake aliyopewa na akajibu: "@aziz.ki.10 kaka yangu endelea kufunga na kufanya unayoyafanya katika ubora wako kaka."


Wakati Guede akifunga bao la pili, Yanga ilishatangulia kwa bao la kwanza lililofungwa na Aziz Ki kwa njia ya penalti baada ya nyota huyo wa Burkina Faso kuangushwa ndani ya boksi na beki anayeinukia wa Simba, Hussein Kazi.


Simba ilifunga bao la kufutia machozi kupitia kwa Michael Koublan ambaye aliipokea kwa utulivu mkubwa pasi ya kiungo fundi wa boli, Clatous Chama na kumlambisha nyasi beki, Ibrahim Bacca huku Bakari Nondo Mwamnyeto akimsindikiza kwa macho wakati akimtungua kipa Djigui Diara wa Yanga.


Hii ni Dabi ya Kariakoo Episode 3 msimu huu, baada ile ya awali iliyomalizika kwa suluhu na Yangu kutolewa kwa penalti katika michuano mipya ya ufunguzi wa msimu kule Tanga ambako Wekundu wa Msimbazi walitwaa Ngao ya Jamii na kisha ile Episode 2 ambayo Simba ilifungwa 5-1 Novemba 5, 2023.


Ushindi wa Kariakoo Dabi Episode 3 umeifanya Yanga kujiimarisha kileleni mwa msimamo katika kampeni ya kuwania taji lake ya tatu mfululizo na la 30 la kihistoria la Ligi Kuu ikifikisha pointi 58 baada ya mechi 22.


Simbe imebaki katika nafasi ya tatu ikiwa na pointi 46 baada ya mechi 21, ikipitwa pia na. Azam FC iliyo katika nafasi ya pili ikiwa na pointi 54. Simba imebakisha mechi 9 kumaliza msimu, Yanga mechi 8, Azam mechi 6.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad