Benchikha na Gamondi Waanza Msako Upya....


Vikosi vya Simba na Yanga juzi usiku vilikuwa uwanjani kumalizana na vigogo wa soka Afrika, Al Ahly ya Misri na Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini katika mechi za marudiano ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika, lakini makocha wa timu hizo wakianza hesabu mpya ya kuvisuka vikosi hivyo.

Yanga ilikuwa Uwanja wa Lotfus Versfeld, jijini Pretoria kumalizana na Mamelodi wakati Simba ilikuwa Cairo kuumana na watetezi wa taji la michuano hiyo, Al Ahly na bila shaka matokeo ya mechi hizo tayari unayo.

Bila kujali matokeo ya mechi hizo makocha wa timu hiyo, Abdelhak Benchikha wa Simba na Miguel Gamondi wa yanga kila mmoja alishaanza mawindo ya usajili kwa ajili ya msimu ujao wakilenga eneo moja.

Tuanze na Simba ambayo imekuwa ikisaka rekodi mpya ya kutinga nusu fainali kwa misimu mitano, kocha Benchikha amefunguka kama kuna kosa hataki lijirudie msimu ujao ni kikosi kukosa mastraika wa maana.

Benchikha ambaye rekodi yake mbele ya Ahly imekuja kutibuliwa akiwa Simba baada ya kupoteza mechi ya kwanza kwa kulala 1-0 Kwa Mkapa, aliliambia Mwanaspoti kwamba Simba haikuwa timu iliyohitaji kusubiri matokeo ya mechi ya pili kujua hatima yake, hatua ambayo imesababishwa na ubutu wa eneo la mwisho.

“Kuna maeneo tumeimarika, lakini bado eneo la mwisho. Kama tungetumia nafasi kwenye mechi iliyopita kule Tanzania nadhani leo (jana) hesabu zetu hapa (Misri) zisingekuwa hizi ambazo tunazo sasa,” alisema.

“Sitarajii tutakuwa hivi tena kwa msimu ujao ushindi wa timu unaamuliwa kwa kufunga mabao. Tunahitaji watu wenye ubora mkubwa huko mbele. Unapocheza mechi kubwa kama hizi dhidi ya timu zenye ubora mkubwa kama hizi kuanzia hapa huhitaji nafasi kumi kufunga bao.

“Niliwahi kushinda mbele ya Ahly, lakini ilikuwa ni nafasi moja tu iliyoamua mchezo. hHata Simba imewahi kuifunga Ahly mara mbili, lakini ni nafasi moja tu iliamua mechi kwa kila mchezo. Tunahitaji watu bora zaidi kwenye eneo la mwisho.”


Simba ilisajili washambuliaji wawili dirisha dogo la usajili Fredy Kouablan na Pa Omar Jobe ambao katika mechi tatu za Ligi ya Mabingwa Afrika walizocheza kabla ya jana usiku wamefunga bao moja pekee.

Jobe ndiye aliyefunga kwenye ushindi wa Simba nyumbani wa mabao 6-0 dhidi ya Jwaneng Galaxy huku mwenzake akijitafuta.

Nyota hao walitua Msimbazi kuchukua nafasi za Moses Phiri aliyetolewa kwa mkopo katika klabu ya Power Dynamos ya kwao Zambia na Jean Baleke (Al lttihad ya Libya) ambapo wawili hao katika Ligi Kuu walichangia mabao 11, Baleke manane na Phiri matatu.


Kitendo cha nyota waliokuwa na mabao mengi kuachwa na kuletwa kina Pa Jobe kimezua mijadala kwa wadau wa Simba, wakidai mabosi wao waliotoa uamuzi huo walichemsha kitu ambacho hata Benchikha amekiri mambo si mazuri.

Kwa upande wa Yanga, kocha Gamondi ana kilio kama cha Benchikaha akisema licha ya ubora ambao umekuwa ukionyeshwa na washambuliaji Clement Mzize, Kennedy Musonda na Joseph Guede bado wanahitaji watu bora zaidi.

Gamondi alisema wakati timu yake inaelekea mwisho wa msimu moja ya eneo ambalo litakwenda kutazamwa kwa umakini ni kutafuta mshambuliaji ambaye atakuja kuongeza kitu kikubwa zaidi kulinganisha waliopo.

“Tunaweza kufurahia kazi ambayo inafanywa na Clement (Mzize), Musonda (Kennedy) na hata Guede (Joseph) lakini bado tunahitaji kitu kikubwa zaidi endapo mambo yataendelea kuwa kama ambavyo tulivyo sasa. Tunatakiwa kuwa na ubora wa kumaliza mechi kubwa kama hizi,” alisema.

Gamondi alisema atatumia dirisha lijalo baada ya kumalizika msimu kushirikiana na wenzake kusaka mshambuliaji wa maana wa kuibeba timu kama ilivyokuwa kipindi cha Fiston Mayele akiichezea kabla hajaja na kuifikisha fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika msimu uliopita.

Mayele ndiye aliyeibuka kinara wa mabao wa michuano hiyo akifunga saba, mbali na mengine saba aliyofunga katika mechi za awali zikiwamo za Ligi ya Mabingwa Afrika kabla ya kutolewa na Al Hilal ya Sudan na kuangukia Kombe la Shirikisho walikofika fainali na kulikosa taji mbele ya USM Alger ya Algeria iliyokuwa chini ya Benchikha anayeinoa Simba kwa sasa.

Mayele pia ndiye aliyekuwa mfungaji bora wa Ligi Kuu sambamba na Saido Ntibazonkiza wa Simba kila mmoja akifunga 17, lakini akiwa kinara wa mabao wa Yanga misimu miwili mfululizo, kwani msimu mmoja nyuma alifunga 16 na kumaliza wa pili nyuma ya George Mpole aliyekuwa Geita Gold aliyebeba tuzo ya Mfungaji Bora msimu wa 2021-2022.

Msimu huu Yanga washambuliaji wake Musonda na Mzize kila mmoja amefunga mabao matatu Ligi ya Mabingwa zikiwamo mechi za raundi ya awali na makundi, huku Guede aliyetua kwenye dirisha dogo akiwa na bao moja alilofunga katika makundi.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad