Watu saba wa familia moja ya Kiislamu mashariki mwa Uganda wamekamatwa na mamlaka kwa madai ya kumpiga msichana wa miaka 18 ambaye alihudhuria ibada ya kanisa, polisi wamesema.
Msichana huyo anadaiwa kuchapwa viboko 100 na mjoma wake huku wajomba zake wengine watano wakimshikilia chini, tovuti ya habari ya Nile Post iliripoti.
Picha zilizoonekana kuonyesha msichana huyo akipigwa zilisambaa kwenye mitandao ya kijamii, na kuzua hisia kali miongoni mwa Waganda.
Familia bado haijatoa kauli yoyote kuhusiana na tukio hilo.
Wajomba wa msichana huyo walikamatwa pamoja na shangazi yake, ambaye ni mlezi wake mkuu, polisi walisema.
Wataendelea kuzuiliwa wakisubiri uchunguzi, Samuel Semewo, kaimu msemaji wa polisi wa mkoa, alinukuliwa akisema.
Mwakilishi wa eneo hilo wa baraza la kitaifa la Waislamu alisema shambulio hilo ni la kinyama na haliungwi mkono na kanuni za dini, gazeti la Daily Monitor liliripoti.