Kamati ya kufuatilia miandamo ya mwezi ya BARAZA KUU LA JUMUIYA ZA ANSAAR SUNNAH TANZANIA (BASUTA), imewatangazia Waislamu wanaofunga na kufungua saumu kwa kufuata mwandamo wa mwezi unaoonekana na kuthibiti Kishari'ah popote pale duniani ya kwamba jana siku ya Jumatatu tarehe 08 Aprili 2024 ilikuwa mwezi 29 Ramadhan, 1445 Hijriyyah.
Taarifa ya BASUTA ya jioni hii imeeleza kuwa kamati hiyo haijapokea taarifa ya kuthibiti kuandama mwezi wa Shawwal si kutoka ndani ya Tanzania wala kutoka nchi nyingine yoyote ile duniani hivyo tunakamilisha Siku 30 Ramadhan leo Jumanne tarehe 9 Aprili, 2024.
"Kamati imepokea taarifa za kutokuandama mwezi kutoka mamlaka mbali mbali za kutangaza mwezi katika nchi za Saudia, Qatar, U.A.E, Misri, Baharain, Kuweit, Yemen, Lebanon, Palestina, Iraq, Syria" imesema taarifa hiyo
"Kwa taarifa hizi, siku ya Jumatano tarehe 10 Aprili 2024 itakuwa ndiyo mwezi
Mosi Mfungo wa Mosi (Shawwal) 1445 Hijriyyah Sikukuu ya ldul Fitr"
Kamati imefikia maamuzi haya kutokana hadithi iliyopokewa na Imam Bukhari na Muslim (Allah awarehemu) kutoka kwa Swahaba Abu Hureira (Allah amridhie) akieleza kuwa Mtume wa Allah (Allah amshushie rehma na amani) anasema:
"Fungeni kwa kuonekanwa kwake (mwezi) na fungueni kwa kuonekanwa kwake (mwezi). Na iwapo mtagubikwa (msiuone mwezi), basi kamilisheni hesabu ya mwezi siku thelathini".
"Kwa mnasaba huu, uongozi wote wa BASUTA unawatakia Waislamu wote kheri ya Siku Kuu ya ldul Fitr mwaka 1445 Hijriyyah pamoja na kuwahimiza kutimiza kutoa Zakatul Fitr kabla ya kuswali swala ya ldd na pia kusherehekea Sikukuu ndani ya mipaka ya Kishari'ah kwa kujiepusha na yale yote yenye kumuudhi Allah (Subhaahuu Wa Taala)"
"Taarifa hii imethibitishwa na masheikh wajumbe wa Kamati ya BASUTA ya kufuatilia Mwandamo wa mwezi na iwapo tutapokea taarifa tofauti na hizi tulizozipokea wakati huu kuhusu kuandama mwezi, Kamati haitasita kuwajulisheni."