Dube Kaingia Anacheka, Katoka Amenuna TFF

 

Dube Kaingia Anacheka, Katoka Amenuna TFF

Mshambuliaji wa Kimataifa kutoka Zimbabwe, Prince Dube aliyeonekana kuwa na tabasamu usoni shauri lake dhidi ya waajiri wake limesikilizwa leo, Alhamisi na Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) jijini Dar es Salaam kwa muda wa saa mbili na dakika tatu.


Kamati ya Sheria na hadhi za wachezaji ya TFF imekutana leo, Aprili 18, 2024 kupitia mashauri tofauti likiwamo sakata la mshambuliaji huyo anayehusishwa na mipango ya kutaka kujiunga na Yanga, ambaye amejiweka mbali na klabu hiyo akitaka kuondoka kwa madai mbalimbali yakiwemo ya kimkataba.


Dube aliiandikia TFF barua kulalamika kuhusiana na mkataba wake mpya na Azam FC kwamba kuna vitu haviko sawa kwa hiyo hautambui. Nyota huyo anadai kuwa na mkataba na Azam FC wa hadi mwishoni mwa msimu huu (2023-24) na sio hadi 2026 kama ilivyoripotiwa na waajiri wake.


Katika kesi hiyo iliyoanza leo, Azam FC iliwakilishwa na wakili wa kimataifa kutoka Ureno kwa njia ya mtandao ambaye jina lake halikutambulika mara moja kutokana na usiri wa kamati hiyo ya TFF inayoongozwa na Mwenyekiti, Said Soud.


Ilikuwa hivi, ikiwa ni siku ya kusikilizwa kwa mashauri mbalimbali ya wachezaji, wajumbe wa kamati hiyo ya TFF ndio waliokuwa wa kwanza kufika katika ofisi za TFF zilizopo kwenye Uwanja wa Karume kuanzia saa 3:30 asubuhi, huku wakipishana dakika chache licha ya mvua ndogo kunyesha walionekana kupata usaidizi wa watumishi wengine wakati wakishuka katika magari yao.


Wakiwa na mafaili waliingia katika chumba maalumu na ndipo dakika 40 baadaye magari aina ya Subaru Forester nyeupe na Nissan ikifuata nyuma yaliingia katika makao makuu ya shirikisho la soka nchini na kuegeshwa, alionekana mwanasheria na Respicius Didas akiwa wa kwanza kushuka kisha kufuata taratibu nyingine huku Dube akisalia katika gari jingine kati ya hayo bila kufahamika.


Hatua kwa hatua mashauri ya wachezaji yalianza kusikilizwa na mara mvua ikakata na ndipo ulipofika muda wa Dube ikiwa ni saa 6:00 mchana, mmoja wa wajumbe (wa kike), alitoka nje na kuongea na mwanasheria wa mshambuliaji huyo ambaye naye alienda kumchukua mteja wake kwenye gari.


Akiwa amevalia tisheti, jeans na kofia, Dube alionekana mwenye tabasamu wakati akiingia kwenye chumba maalum ambacho kilikuwa kikitumika akiwa mlangoni alivua kofia, kisha mlango ukafungwa.


Tofauti na alivyoingia Dube alitoka huku lile tabasamu likionekana kuyeyuka, akiongozwa na mwanasheria wake uelekeo wa magari walipopaki kabla ya kusema chochote juu ya kilichoendelea.


DUBE AFUNGUKA


Dube hakuwa mtu mwenye maneno mengi, alisema, "Tusubiri kuona nini kitatokea, naamini kila kitu kitaenda vizuri."


Kwa upande wa mwanasheria wake, Didas amesema anaamini kamati itatenda haki kwa mteja wake.


"Siwezi kusema nini tumeongea ndani lakini suala ni kuhusu mkataba, tunachojua mteja wangu mkataba wake unaisha mwisho wa msimu, tumejieleza na wao wameeleza tunasubiri wapitie na kuona nini tena kinaweza kufuata," alisema.


Dube na Mwanasheria wake walitoka kwa pamoja saa 8:10 makao makuu ya shirikisho hilo huku kamati ikiendelea na mashauri mengine.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad