Clatous Chama a |
Kiungo wa Simba Clatous Chama anayemaliza mkataba mwishoni mwa msimu huu ametajwa kuhusisha na Yanga, zikiwa zimebaki wiki chache kabla msimu haujamalizika.
Mkataba wa Chama na Simba unafikia mwisho mara baada ya msimu huu kumalizika, na inaelezwa kuwa Simba bado haijafanya maamuzi ya mwisho kama itamuongeza mkataba mpya au vinginevyo huku yeye mwenyewe akiendelea kupiga kazi.
Taarifa kutoka ndani ya Yanga, zimeliambia Mwananchi kuwa Yanga tayari imeshaanza mazungumzo ya siri na kiungo huyo raia wa Zambia.
Chanzo hicho kimesema hadi sasa utata kati ya mchezaji huyo na Yanga ni urefu wa mkataba, huku mwenyewe akitaka apewe miaka miwili na klabu hiyo imejiandaa kumpa mwaka mmoja tu wakiamini atakuwa msaada kwao kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa mwakani kutokana na uzoefu wake.
"Tusubiri kuona kipi kitatokea kwenye mazungumzo ambayo yanaendelea, ila Chama mwenyewe ameonyesha kukaribia kukubali kuja kuvaa jezi yetu msimu ujao na sisi Yanga atatufaa sana," alisema bosi huyo wa Yanga aliyeongeza;
"Tunachotaka msimu ujao tuwe na kikosi kizito zaidi ya msimu huu yaani huyu anayetoka wa moto na anayeingia wa moto zaidi ili ushindi uwe uhakika kuzidi tulichofanya msimu huu."
Ukiachana na Yanga pia Azam nao wako njia hiyohiyo, ikivizia saini ya kiungo huyo lakini inaelezwa mwenyewe amewaweka matajiri hao wa Chamazi kama chaguo la mwisho kutokana na kukosa nguvu ya ushiriki wao kimataifa lakini pia kupigania mataji.
Msimu huu Chama ameshaifungia Simba jumla ya mabao 10 yakiwemo saba ya Ligi Kuu Bara na matatu ya Ligi ya Mabingwa Afrika, huku asisti zikiwa nane, zikiwamo saba za Ligi Kuu na moja ya Ligi ya Mabingwa.