Job: Tumeshawasoma Hao Mamelodi, Wanafungika Vizuri tu

 

Job: Tumeshawasoma Hao Mamelodi, Wanafungika Vizuri tu

Wakati Yanga ikijiandaa na safari ya kwenda Afrika Kusini kwaajili ya mchezo wa marudiano na Mamelodi Sundowns, beki wa kikosi cha Wananchi, Dickson Job amesema mwendo ni uleule.


Nahodha msaidizi huyo ni miongoni mwa wachezaji wa kikosi cha kwanza waliocheza mchezo wa kwanza kwenye uwanja wa nyumbani (Benjamin Mkapa) ambao ulimalizika kwa matokeo ya 0-0.


Akizungumza nasi, Job alisema kwa sasa presha imepungua kwani wameshatoa joto la hofu katika mchezo wa kwanza.


Alieleza kuwa marudiano kwao ni mchezo wa muhimu kwani baada ya kuwasoma sasa wanakwenda kutafuta matokeo ili kutinga nusu fainali.


"Katika mchezo uliopita, tulicheza vizuri timu nzima. Malengo yetu sasa ni kwenda kurudia kucheza kwa ubora ule au zaidi mechi ya ugenini, tunafahamu haitakuwa rahisi lakini tupo hapa kuipigania Yanga na taifa letu," alisema Job, ambaye katika mechi hiyo alicheza kulia ambako mabeki Yao Kouassi na Kibwana Shomary walikosekana kutokana na kuwa majeruhi.


"Kwa muda mrefu binafsi nilikuwa na kazi ya kuwafuatilia washambuliaji wao lakini pia kama timu tumekuwa na vipindi ya kuwangalia wanavyocheza mechi mbalimbali, tutakwenda ugenini kupambana zaidi ili tufanikishe malengo yetu."


Mabingwa wa kombe la michuano mipya ya klabu Afrika ya AFL, Mamelodi, walitawala mchezo kwa asilimia 69 dhidi ya 31 za Yanga, lakini walikuwa ni wanajangwani waliotengeneza nafasi nyingi zaidi za kufunga wakipiga mashuti manne yaliyolenga lango dhidi ya mawili ya Masandawana.


Yanga itashuka uwanjani huko Pretoria kusaka hatima yake ya kuandika historia ya kufuzu nusu fainali ya LIgi ya Mabingwa Afrika kwa mara ya kwanza katika mechi itakayochezwa Ijumaa hii Aprili 5 kuanzia saa 3:00 usiku.


Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad