Kocha Benchikha Anamtamani Kocha Gamondi Mechi ya Simba na Yanga

 

Kocha Benchikha Anamtamani Kocha Gamondi Mechi ya Simba na Yanga

Wakati mechi ya watani wa jadi inakaribia, kikosi cha Simba kinaendelea kujifua mjini Zanzibar, huku silaha ya viongozi wa timu hiyo kwa sasa ikiwa ni kuwa kimya, lakini wakiwa kwenye mikakati mikali kuhakikisha inashinda.


Hayo yakiendelea, Kocha Mkuu, Abdelhak Benchikha, amesema kazi yake ya siku hizi mbili tatu ni kuwaweka vizuri wachezaji wake kisaikolojia na kuwapa mbinu mbalimbali za kumalizia mipira kwa kuiweka ndani ya nyavu ili kuibuka kidedea Jumamosi ijayo kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.


Habari kutoka ndani ya klabu hiyo, zinasema viongozi wa klabu wanaelewa kila kitu kinachoendelea kuwa waandishi wa habari, wachambuzi na hata mashabiki wa soka wanaipa nafasi kubwa Yanga, huku wakiibeza timu yao, na hilo limewapa nafasi ya kukaa kimya bila kuongea neno lolote, lakini wakiwa kwenye mikakati mbalimbali kuhakikisha wanashinda mechi hiyo na kujiongezea pointi tatu.


"Mikakati inayofanywa ni kuzuia hila na mbinu zozote chafu ambazo zinaweza kutumika ili kupoteza mechi, kwa sababu wanaamini hata mechi iliyopita hawakufungwa mabao 5-1 kwa kuzidiwa sana na watani zao, ila kuna mbinu ambazo walizigundua mara tu baada ya mechi," alisema mtoa habari.


Alisema moja ya mikakati hiyo ni kuiondoa timu Dar es Salaam na kuipeleka Zanzibar, hivyo kubainisha kuwa mechi ya Jumamosi haitokuwa rahisi kwa Yanga kama wengi wanavyodhani.


"Mechi ile kuna baadhi ya wachezaji waliondoka kambini, hawakulala kambini kuelekea siku ya mechi, wakarejea asubuhi, lakini cha kustaajabisha, pamoja na baadhi ya wadau wa karibu kutaka wasichezeshwe kwa sababu wamekiuka miiko ya kambi, lakini walicheza na kile ndicho kilichotokea, safari hii kitu cha kwanza ni kuwaondoa mjini kwanza, mengine wanaendelea kuyafanyia kazi, kwa hiyo nakuhakikishia viongozi na wadau wengine walioletwa kuongeza nguvu wapo mzigoni, mechi haitokuwa ya kitoto kama watu wanavyodhani, tahadhari zote zimechukuliwa,"kilisema chanzo hicho.


Kwa upande wa Benchikha, amesema tatizo kubwa analoliona ni umaliziaji tu hakuna kingine, akaenda mbali zaidi akisema ni tatizo la nchi nzima, kwani ameangalia hata baadhi ya mechi za ligi na kugundua udhaifu wa washambuliaji wengi wanaocheza soka nchini.


"Tunafanya kila kitu, lakini hatuweki mpira wavuni, hii ni shida, nimeamua kubadilisha kidogo mbinu na mfumo ili kuwarahishia kazi ya kufunga, siku hizi chache ambazo tupo hapa nawafua wachezaji wangu ili wawe makini wanapokuwa mbele ya lango," alisema Benchikha raia wa Algeria.


Timu hizo zinakwenda kucheza mechi ya 'dabi', Yanga ikiwa inaongoza ligi kwa pointi 55 ambayo itakuwa mwenyeji wa mchezo huo, huku Simba, inayoshika nafasi ya tatu kwa pointi 46, ikiwa mgeni kwenye mechi hiyo itakayopigwa Jumamosi kuanzia saa 11:00 jioni.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad