Kocha: Mzize Anajua Boli, ila ana Tatizo Hili

 

Kocha: Mzize Anajua Boli, ila ana Tatizo Hili

Kocha Mkuu wa Dodoma Jiji, Francis Baraza amekiangalia kikosi cha Yanga na kukiri hakuna wa kuizuia kubeba ubingwa, lakini akasema straika chipukizi wa timu hiyo, Clement Mzize anajua sana boli, ila ana tatizo moja tu la kukosa utulivu anapokuwa mbele ya lango na kutakiwa alirekebishe awe mtamu zaidi.


Akizungumza na Mwanaspoti, Baraza alisema Mzize ni mchezaji mzuri na mkubwa kama atafanyia kazi mambo kadhaa “Sioni akicheza Tanzania, ni mchezaji mzuri.”


“Kwanza anatakiwa kufanyia kazi suala la umaliziaji, namshauri aangalie video za mchezaji wa zamani wa Manchester United, Javier Hernandez ‘Chicharito’ na kujaribu kufanya mazoezi ya kufunga akiwa mwenyewe bila kipa langoni,” alisema Baraza na kuongeza;


“Mzize ni mshambuliaji mzuri aache kukokota sana mipira, anafanya hivyo kwa sababu ana nguvu na uwezo wa kusumbua mabeki, shida ni moja tu katika kumalizia...ukiangalia kwa washambuliaji waliopo msimu huu yeye ndiye aliyetengeneza nafasi nyingi.”


Baraza alisema hakuna mshambuliaji aliyetengeneza nafasi nyingi za kufunga kama Mzize akiwa ndani ya boksi, ila shida ni kukosa umakini wa umaliziaji na kwamba akiongeza ubora zaidi katika kumalizia atatisha kwa nafasi anazozipata.


Alisema ili Mzize aweze kuwa bora anatakiwa kukaa kwenye maeneo na kutumia nafasi bila kutafuta ushindani na mabeki ndani ya 18 huku akikiri kuwa endapo atafanyia kazi mambo hayo anamuona akiondoka Tanzania.


“Mzize akifanyia kazi hayo mambo niliyoyasema hapo sioni akicheza soka la Tanzania na mimi nipo upande wake siku zote, nampongeza kocha Miguel Gamondi kwa kuendelea kuamini katika kipaji hicho kwa kumpa nafasi,” alisema na kuongeza;


“Licha ya mashabiki kumzomea kutokana na kukosa nafasi lakini kocha Gamondi amewapa kisogo ameendelea kumpa nafasi na anafanya vizuri juzi katuadhibu kwenye mechi ya Kombe la Shirikisho, ameukokota mpira katikati ya mabeki na kufunga ni mchezaji mwenye nguvu na anajiamini,” alisema.


AIPA UBINGWA YANGA


Katika hatua nyingine, Baraza alisema Yanga ina timu iliyokamilika kila eneo huku akitaja mchezaji mmoja kila nafasi kuwa wana kila sababu ya kuipa ubingwa timu.


“Tumekutana na Yanga katika mechi za ligi na FA zote tumepoteza licha ya kucheza mchezo mzuri dhidi yao, sababu kubwa ni kutokana na namna walivyo na wachezaji wazuri na wazoefu,” alisema kocha huyo wa zamani wa Biashara Utd na Kagera Sugar na kuongeza;


“Yanga wana Djigui Diarra langoni, ni kipa mzuri na mzoefu, Ibrahim Abdallah ‘Bacca’ beki mzuri, Khalid Aucho na Jonas Mkude eneo la kiungo wote ni wazoefu na wanaipambania timu kuhakikisha inapata matokeo.


“Ukiachana na eneo hilo ambalo kwa kiasi kikubwa limefanya kazi nzuri kumlinda Diarra pia wana Stephane Aziz Ki, Pacome Zouzoua na Mzize ambaye licha ya uchanga wake lakini anakomazwa na ubora wa wachezaji anaocheza nao.”


“Wameshajijenga kitimu na ndio maana tunashuhudia kuna timu zinafungwa mabao 5-0 na zisipoangalia na kujiimarisha zaidi kuna timu zitafungwa mabao saba kwani muunganiko wa timu hiyo sioni watu wa kuwazuia kutwaa taji la msimu huu.”

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad