KLABU ya Simba imeweka wazi kuwa hawana mpango wa kuachana na kocha wao, Abdelhak Benchikha na tayari wameshakutana kwa ajili ya kujadili tathimini ya maboresho ya kikosi cha timu hiyo kwa msimu ujao wa Mashindano.
Kauli hiyo ni baada ya kuwepo kwa taarifa katika mitandao mbalimbali juu ya kocha Benchikha yupo hatarini kupoteza kubarua chake hicho kwa kutupiwa virago ndani ya timu hiyo ya Simba.
Meneja wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally amesema hakuna ukweli juu ya kutaka kumtimua au kusitisha mkataba na Benchikha na kuendelea kumuamini.
Amewataka mashabiki kutulia kwa kipindi hiki cha mpito na kuimarisha nguvu na mshikamano kwa ajili ya kuimarisha timu yao kwa msimu ujao kulingana na mapendekezo ya benchi la ufundi linaloongozwa na Benchikha.
“Hatuna mpango huo wa kumuondoa au kuachana na Benchikha, wanasimba wanatakiwa kupuuza taarifa zilizosambaa kuhusu kocha wetu, bado yupo kwenye mipango ya klabu na sasa wazo mikakati yetu ni kuboresha na kujenga timu ya msimu ujao lakini pia kuhakikisha tunafanya vizuri katika michezo iliyopo mbele yetu.
Benchikha yupo sana na leo mchana alikuwa sehemu ya timu iliyoenda Visiwani Zanzibar kwa ajili ya michuano ya kombe la Muungano ikiwa ni sehemu ya mipango ya kuhakikisha tunafanikiwa kushinda kombe hilo,” amesema Ahmed.
Ameongeza kuwa kikosi kipo vizuri na wachezaji wote wako salama na wako kwenye msafara huo kasoro wawili, Beki Shamari Kapombe aliyeumia kwenye mazoezi ya kujianda na mchezo dhidi ya Yanga.
Ahmed amesema mchezaji mwingine ambaye hajaambatana na timu ni kiungo Sadio Kanoute majeraha aliumia kwenye mchezo wa na Yanga wikiendi iliyopita.
Ameeleza kuwa wachezaji wapo tayari kwa ajili ya michuano hiyo ya kombe la mapinduzi kwa kufanya vizuri katika mchezo wa kwanza wa nusu fainali dhidi ya KVZ ya Visiwani humo.
Simba kesho inamenyana na wenyeji, KVZ katika Nusu Fainali ya Kombe la Muungano, Uwanja wa New Amaan Complex visiwani, ZanzÃbar wakati Azam FC itaanza na KMKM Alhamisi na Washindi wa mechi za Nusu Fainali watakutana katika Fainali Aprili 27 hapo hapo Amaan Complex.