Dar es Salaam. Mahakama Kuu masjala ya Dar es Salaam, imetoa kibali kwa askari watatu wa zamani Jeshi la Polisi nchini, waliofukuzwa kazi mwaka 2022, kufungua maombi dhidi ya Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP), kupinga kufukuzwa kwao kazi.
Polisi hao wa zamani waliokuwa wakifanya kazi uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) Jijini Dar es Salaam ni Rabson Mosha na Amelda Honga waliokuwa na cheo cha Koplo na Denice Kasimbazi aliyekuwa na cheo cha Konstebo.
Uamuzi wa kuwapa kibali cha kufungua maombi ya kuiomba mahakama ipitie upya uamuzi wa kufutwa kwao kazi wakisema uligubikwa na uharamu kisheria, ukiukwaji wa kanuni na haukuwa wa haki, umetolewa Aprili 9, 2024 na Jaji Arnold Kirekiano.
Kupitia maombi namba 6575 ya mwaka 2024 kati ya waombaji hao dhidi ya IGP kama mjibu maombi wa kwanza na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) kama mjibu maombi wa pili, Jaji amewapa waombaji muda wa siku 14 wawe wamefungua maombi yao.
Jaji Kirekiano amesema amezingatia kuwa uamuzi wa kuwafuta kazi uliwaathiri maofisa hao, kwa hiyo wana masilahi ya kuomba kufungua maombi ya mapitio ya kimahakama ili waweze kupinga kufukuzwa kwao kazi ndani ya Jeshi la Polisi.
Mwaka 2022, maofisa hao walishitakiwa katika mahakama ya kijeshi kwa makosa mawili ya kufanya kitendo ambacho ni kinyume cha mwenendo mwema wa Jeshi la Polisi, kuomba na kupokea rushwa kinyume cha kifungu namba 106.5 cha PGO.
Walipatikana na hatia na kufukuzwa kazi ambapo hawakuridhika na maamuzi hayo wakakata rufaa kwa IGP lakini rufaa yao ikatupwa na wakajulishwa Oktoba 5,2023, na sasa wamebisha hodi mahakamani ili wapewe kibali kufungua maombi hayo.
Wanadai kuwa uamuzi wa IGP wa kuwafuta kazi ulikuwa haramu kisheria, kwa kuwa haukuzingatia makosa ya kisheria yaliyofanywa katika uamuzi wa mahakama ya Kijeshi iliyoendeshwa na Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP), Geremia Shila.
Pia wanalalamika kuwa uamuzi wa IGP kubariki uamuzi wa kuwafuta kazi uliofikiwa na ACP Shila, haukuwa wa haki na haukuzingatia utaratibu uliowekwa na sheria kwa kuwa hakukuwa na ushahidi wowote dhidi yao.
Mbali na hoja hiyo, polisi hao wanaowakilishwa mahakamani na wakili Peter Majenjela wamesema uamuzi huo wa ACP Shila kwa ujumla wake ulikuwa sio sahihi kwa vile haukuzingatia kanuni za usikilizwaji wa mashauri katika mahakama ya kijeshi.
IGP na AG katika maombi hayo ya kibali cha kufungua maombi ya mapitio ya uamuzi wa kuwafuta kazi, walitetewa na wakili wa Serikali Pauline Mdendemi ambaye amesema hawana kipingamizi kupewa kibali hicho na ndio maana hawakuwasilisha kiapo kinzani.
Katika uamuzi wake wa kuwapa kibali, Jaji Kirekiano amesema katika wasilisho la pamoja la kuomba kibali, waombaji hao wameeleza sababu watakazoziegemea wakipewa kibali hicho kuwa ni pamoja na ukiukwaji wa kanuni, sheria na upendeleo.
“Katika hatua hii, mahakama haihitaji kujadili uhalali au kinyume chake juu ya malalamiko yao ya kufutwa kazi. Inatosha kwamba waombaji wameonyesha kuwa watawasilisha hoja za kupinga kufutwa kwao kazi,”amesema Jaji Kirekiano.
Jaji KIrekiano amesema msimamo wa sheria ni kwamba kibali cha kuomba kuruhusiwa kufungua maombi ya mapitio ni lazima yawasilishwe miezi sita baada ya tarehe ya mwenendo au kitendo ambacho kinalalamikiwa na waombaji wa kibali.
“Waombaji walifungua maombi haya ndani ya muda wa miezi sita kuanzia Oktoba 5,2023 uamuzi ulipotolewa hadi Februari 26,2024 maombi yalipofunguliwa,”alisema Jaji Kirekiano katika uamuzi wake huo alioutoa Aprili 9,2024.
Jaji alisema ameona maombi hayo ya kupewa kibali cha kufungua maombi ya kupinga kufutwa kwao kazi yana mashiko, hivyo anatoa kibali kwao na kuwataka wawe wamefungua maombi hayo ndani ya siku 14 tangu siku uamuzi huo alipoutoa.