Sina shaka wengi wetu tunatambua kuwa Ndoa ni muungano kati ya watu wawili au zaidi unaokubaliwa na kuheshimiwa na jamii huku tukio hilo la ndoa likiitwa harusi, ambapo kabla ya ndoa hiyo huwa kuna kipindi cha uchumba kwa wawili waliokubaliana (mume na mke) kuchunguzana tabia na kujifunza au kujuana zaidi baina yao.
Lakini endapo wawili hao walioingia katika makubaliano ya ndoa watasitisha na kuivunja ndoa yao kisheria, hali hii huitwa talaka kwa Mwanamke na Mwanamume kusitisha maisha ya pamoja kama mume na mke.
Mahuasiano yamejaa visa vingi, lakini vipo vya kushangaza na hata vile vya kusisimua au kukuachia tafakari ya mazingira husika na usipate majibu sawia, kwani mwaka wa 2011 Mwanamume aliyejulikana kwa jina la Antonio raia wa Italia akiwa na umri wa miaka 99 alimpa talaka mke wake Rosa aliyekua na miaka 97.
Antonio na Rosa waliodumu katika ndoa kwa miaka 77 walitalikiana baada ya mume kugundua mkewe aliwahi kuchepuka miaka 60 iliyopita, na licha ya Rosa kukiri na kuomba msamaha lakini jamaa aligoma.
Ilikuwa ni siku chache kabla ya Krismasi miaka ya 1940, Antonio katika pekua pekua yake kwenye makabrasha yaliyokuwa kwenye droo ndani ya nyumba yao, alikuta barua za zamani za mapenzi zilizotumwa kwa mkewe Rosa.
Baada ya kumuuliza mkewe Rosa, inasemekana alikiri kila kitu lakini hakuweza kumshawishi mume wake kufikiria upya uamuzi wake, kwani alipata maumivu makali kutokana na usaliti huo alioufanya miaka 60 nyuma.
Katika hati za Mahakama ya Italia, Antonio aliwasilisha kesi ya talaka kwa mkewe na kufanya waingie katikia rekodi ya watalaka wakongwe zaidi duniani na kuvunja rekodi ya awali ya Bertie na Jessie Woods, ambao wote walikuwa na umri wa miaka 98 walipotalikiana.
Ama kweli, ingawa wengi huapa kubaki na wenzi wao hadi ‘kifo kitakapowatenganisha’, lakini ni wazi kuwa si kila wanandoa huifika ahadi yao, kwani katika maisha ya ndoa kuna faida na changamoto pia hili lazima kila mmoja alifahamu na ndio maana hata wakati wa kufunga ndoa huwa kuna kiapo kikibainisha utavumilia kwa shida na raha.
Kwenye maisha ya ndoa kuna mambo mengi lakini kubwa ni uthamani wa mwenza wako, kwani hakuna anayetamani kuonekana anachukuliwa kawaida, ndivyo ilivyo na huu ni uhalisia kwani haijalishi mnapitia Matatizo au changamoto kiasi gani, haijalishi umekosewa kiasi gani lakini ione thamani ya mwenza wako.
Makosa hutokea kwa watu wote, hivyo kuwa na uelewa kwamba matatizo katika ndoa hayatakufanya kuiondoa thamani ya mwenzi wako kwa kumdharau, kumshushia thamani yake na kumchukulia kawaida na hata kumsaliti kwani hapo ndipo palipo na anguko baya.
Lakini pia tambua wakati wa kipindi cha matatizo, changamoto, mgogoro au ugomvi na mwenzi wako unapotokea epuka kutumia udhaifu wake kama silaha yako ya kumfedhehesha, kumuaibisha na kumdhalilisha, maana kuna tofauti kubwa kati ya kuficha ukweli muhimu na kusema kila kitu kinachokuja akilini mwako, hasa wakati mnapotofautiana.
Ni lazima kuifanya ndoa yako kuwa kipaumbele chako wakati wote, ingawa hili ni jambo rahisi kulisema lakini linaweza kuwa ni gumu kulifanya licha ya ukweli kuwa katika utafiti uliofanywa na Mwanasaikolojia na mshauri nasihi wa mahusiano (John Lennon), aliesema sababu inayochangia kiwango kikubwa cha talaka katika maisha ya ndoa ni kutanguliza mambo mengine kuliko mwenzi wako.
Huduma ya ushauri nasaha hasa katika kipindi cha matatizo, migogoro, ugomvi usiokoma, kutokuelewana katika maisha ya ndoa ina msaada mkubwa sana, kwani si kila Matatizo, ugomvi, migogoro inapotokea mwisho wake huwa ni maamuzi ya kuachana au kupeana Talaka.
Kuna ugomvi mwingine kabla ya kufanya maamuzi ya talaka au kuachana, atahitajika mtu wa tatu ambaye ni mshauri ama Mwanasaikolojia, au hata Wasimamizi wa ndoa, Wazazi au Viongozi wa Dini ambapo kupitia wao kutakusaidia kujua ni nini chanzo cha tatizo lililopo katika ndoa yenu, lakini pia utajifunza jinsi ya kukabiliana na tatizo kwa njia kujenga na si kubomoa.
Ikumbukwe kuwa ndoa ina faida nyingi. Na inaarifiwa kuwa watu walio katika ndoa huishi miaka mingi, hawapatwi na magonjwa ya kawaida kama homa kwa urahisi, wana amani na utulivu wa nafsi na hata kihisia wapo vizuri na pia watu walio katika ndoa hawana matatizo ya msongo wa mawazo na unyongovu.
Wataalamu wa masuala ya ndoa wanasema hata kitendo cha kuushika mkono wa mpenzi wako pekee, uwezekano wa kupatwa na shinikizo la damu hupungua kwa asilimia kubwa, kwani kuna visa vichache sana vya kifo kwa watu walioko katika ndoa kuliko wale wasiokuwepo kwenye ndoa.
Kama mtu ataenenda kiyume na haya na kuongozwa na hisia, basi kuna uwezekano mkubwa wa kuharibu ndoa yake kiasi anaweza hata kuchepuka na hapo atapata upande wa uzuri na upande wa ubaya, ila katika kufanya maamuzi basi ni vyema kuegemea upande wenye mazuri zaidi kuliko mabaya, kwani uchunguzi mdogo nilioufanya na usio rasmi, suala la kuchepuka lina madhara makubwa.
Tukumbuke kwamba kuchepuka ni aina nyingine ya usaliti anaoufanya mtu kwa mpenzi wake, japo wahenga walinena acha michepuko baki njia kuu, lakini michepuko hutokea katika nyanja zote za mahusiano, kuanzia kwenye uchumba hadi kwenye ndoa, sababu huwa ni nyingi na viwango hutofautiana lakini hili likitokea huwa si jema.
Hata hivyo, fahamu kwamba ukichepuka kuna uwezekano wa kuambukizwa magonjwa ya zinaa kama kinga haitatumika, utasahau au kuacha kabisa kuhudumia familia na kumuhudumia mchepuko, kwani wapo waume za watu wanaishi nyumba za kupanga na familia zao, ila wamewajengea nyumba michepuko yao au wengine wamewanunulia magari, huku mke wake akiwa anahangaika na daladala.
Ukichepuka pia unaishi kwa hofu na mwenza wako, kwani nafsi itakusuta kwa hofu kuwa ya siri ya mchepuko inaweza kuvuja, gharama zitapanda kugharamikia familia na mchepuko, utakosa muda wa kuwa karibu na familia yako na hutakuwa huru na mwenzi wako, kwani kuna kitu unakificha na hutakuwa huru na mawasiliano yako, japo wapo waliokubuhu ambao huona jambo hilo ni kawaida na wayaishi maisha hayo, kama ni uhalisia ingawa madhara ya mbele huwa ni makubwa.
Katika tukio la Antonio na Rosa la kuachana uzeeni lina mambo mengi, wapo watakaoona ni sawa na wapo watakaoona amekosea, lakini ikumbukwe kuwa usaliti huutesa moyo bila kujali umri wa muhusika kwani ni lazima maumivu yaje nafsini.
Tatizo hapa sio umri wa kuachana, bali ni hisia kupanda na kumkumbusha mambo mengi katika maisha ya mapenzi mtendewa akikumbuka kwamba ni mkewe na mpaka kuwa katika umri huo atawaza wamepitia mambo mengi na mkewe ni moyo wake na aliuamini. Hilo linaweza kumtafakarisha kwamba amesalitiwa mara ngapi bila ushahidi wa barua na je kama si barua ina maana angeishi bila kujua hadi kifo?
Inaumiza kwa mtendwa japo busara zilitakiwa kutumika kutokana na uhalisia kwamba kusamehe ni jambo jema kuliko kuharibu, na hapa tunapata dhana mbili kwamba kuna faida na hasara japo jawabu ni kuwa usaliti ni usaliti tu na hauwezi acha kuleta maumivu na ukweli ni kuwa mapenzi hayana umri. Ingawa binafsi siungi mkono babu kumuacha bibi, lakini nakubalinana naye kwamba alipata maumivu.