Aliyewahi kuwa Mwenyekiti wa Yanga, Yusuf Manji, Jumamosi iliyopita alishuhudia mchezo wa Dabi ya Kariakoo kati ya Yanga na Simba na kusema: “Tatizo la Simba ni mtu huyu.”
Yanga ikiwa mwenyeji kwenye mchezo huo wa Ligi Kuu Bara uliopigwa kwenye Uwanja wa Mkapa jijini Dar es Salaam kuanzia saa 11:00 jioni, ilifanikiwa kuichapa Simba mabao 2-1.
Hii ni mara ya pili Yanga inaibuka na ushindi dhidi ya Simba msimu huu ndani ya ligi, baada ya mchezo wa kwanza kushinda kwa mabao 5-1.
Akizungumza kwenye mahojiano maalumu na Mwanaspoti Jijini Dar es Salaam, Manji ambaye anatambulika ni shabiki mkubwa wa Yanga, alisema kinachoimaliza Simba ni baada ya kifo cha Zacharia Hans Poppe ambaye amewahi kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili wa timu hiyo na kinara wa kundi la Friends of Simba.
Tangu Hans Poppe, amefariki dunia Septemba 10, 2021, Simba imekuwa haina matokeo mazuri, huku Yanga ikionekana kulitawala soka la Tanzania kwa kipindi hicho baada ya kutwaa ubingwa mara zote.
Kabla ya kufariki, Hans Poppe aliiongoza Simba kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara mara nne mfululizo, huku Yanga ikionekana kuhaha kila msimu.
“Unajua wakati nikiwa Yanga, mtu pekee aliyekuwa ananipa wakati mgumu ni Hans Poppe. Huyu jamaa alikuwa anafanya kazi yake kuonesha kabisa kuwa Dabi inatakiwa kuwa na mvuto, alikuwa akizungumza na watu wanamuelewa, alinipa wakati mgumu sana.
“Hata niliposikia amefariki, ukweli kibinadamu nilisikitika sana kwa kuwa alikuwa ni mtu muhimu kwenye soka, lakini nilijua kabisa kuwa Simba inakwenda kupata wakati mgumu na hiki ndiyo kinatokea leo, nafikiri mechi umeiona na msimamo unaonesha hali halisi ilipo Yanga na Simba kwa sasa,” alisema Manji ambaye alidumu kwenye timu ya Yanga kwa miaka 13 kama mfadhili na Mwenyekiti.
Manji ambaye alifanya usajili wa wachezaji wengi mastaa akiwa na Yanga kama mfadhili na baadaye mwenyekiti, amesema pamoja na kwamba walikuwa wanapambana na Hans Poppe kwa ajili ya kuhakikisha timu zao zinapata mafanikio, lakini nje walikuwa marafiki na walikuwa wanazungumza.
“Tulikuwa tunapambana sana uwanjani, lakini tulikuwa marafiki, alikuwa akizungumza lazima nijue amesema nini, huyu alikuwa ana nguvu kubwa sana kwenye soka la Tanzania na alikuwa anaweza kufanya jambo lolote na watu wakamuelewa.
“Nafikiri unakumbuka wakati tulipoichapa Simba mabao matatu hadi mapumziko, baadaye wakaja kurudisha yote. Hapa Hans Poppe alihusika, siwezi kukuambia alifanyaje, lakini nguvu yake ilisababisha Simba wakapata sare kwenye huo mchezo, alikuwa na ushawishi wa hali ya juu sana kwa wachezaji,” alisema Manji ambaye alijiuzulu nafasi ya Mwenyekiti Yanga Mei 21, 2017.
Manji ambaye mwaka 2012 aligombea Uenyekiti Yanga na kushinda ikiwa ni siku chache baada ya timu hiyo kuchapwa mabao 5-0 na Simba, anasema moja ya usajili ambao anaukumbuka ni wakati alipomchukua kipa Juma Kaseja kutoka Simba, huku Hans Poppe akiwepo.
“Pamoja na uwepo wa Hans Poppe, lakini naamini kuwa niliwahi kumuumiza, nakumbuka Juma Kaseja akiwa na kiwango cha hali ya juu nilimsajili akitokea Simba kwa kitita cha shilingi milioni hamsini, hiyo ni mwaka 2014.
“Huu ndiyo ulikuwa usajili wangu mkubwa zaidi kwa kipindi chote nilichokaa madarakani, lakini pia alifanya kazi kubwa akiwa nasi kwani alitwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara,” alisema Manji ambaye amekuwa akifuatilia soka la Tanzania kwa kipindi chote.
Mbali na Kaseja pamoja na umafia wa Hans Poppe, Manji aliibomoa Simba kwa kuwasajili nyota wengine kama Mrisho Ngassa, Ally Mustapha ‘Barthez’, Kelvin Yondani, Deogratius Munishi ‘Dida’, Athuman Idd ‘Chuji’ na wengineo.
Kwa kipindi cha miaka mitano ambacho Manji alikaa madarakani, Simba haikuwahi kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu baada ya Yanga kuuchukua mara nne (2012/13, 2014/15, 2015/16 na 2016/17) na Azam mara moja (2013/14), baadaye mambo yakabadilika.
POPPE ALIKUWA NANI TANZANIA?
Miongoni mwa mambo ambayo Poppe yalimjengea zaidi jina Simba ni uwezo wake wa kufanya maamuzi ya haraka haswa katika usajili wa wachezaji wa ndani ambapo miongoni mwa mastaa wakubwa wazawa aliowasajili ni Mohamed Tshabalala, Ramadhani Redondo, Haruna Moshi ‘Boban’ na Clatous Chama.
Lakini hata nafasi yake ya Mwenyekiti wa Kamati ya usajili ilimpa umaarufu mkubwa mwanzoni mwa miaka ya 2000 wakati mitandao ya kijamii inaanza kuibuka kwani alikuwa mstari wa mbele kwenye mambo mengi.
Historia ya Hans Poppe inakwenda mbali zaidi ya ushiriki wake wa michezo. Aliwahi pia kuwa ofisa wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) na ni mmoja wa maofisa wa jeshi ambao walikamatwa mwaka 1983, wakituhumiwa kwa njama za uhaini wa kumpindua na kumuua Rais wa awamu ya kwanza, Mwalimu Julius Nyerere.
Historia inasema, Hans Poppe alikuwa miongoni mwa zaidi ya Watanzania 32 waliokamatwa na miongoni mwa washtakiwa 19 waliofikishwa mahakamani na hatimaye kuhukumiwa. Walidaiwa kuwa walikula njama kwa pamoja kutaka kuiangusha Serikali kati ya Juni 1982 na Januari 1983.
Baadhi ya waandishi wakongwe wa habari za michezo wanadai kuwa alipenda Simba tangu ujana wake mwanzoni mwa miaka ya 1970, akiwa kijana mdogo na kwamba mechi iliyomfanya atamke rasmi kuwa yeye ni Simba ilikuwa ni pale Simba walipocheza na watani wao, Yanga Jumamosi ya Juni 23, 1973, ambapo Simba ilishinda 1-0 kwa goli lililofungwa na Haidari Abeid ‘Muchacho’ katika dakika ya 68.