Miili saba ya wanafunzi wa Shule ya Msingi Ghati Memorial iliyoko Murieti jijini Arusha imepatikana katika maeneo tofauti na kukamilisha idadi ya wanafunzi waliokufa maji katika ajali hiyo.
Miii hiyo imepatikana kwa msaada wa uokozi unaofanywa na Jeshi la Zimamoto, Polisi kwa kushirikiana na mkuu wa wilaya pamoja na wananchi.
Wanafunzi hao wamefariki dunia baada ya gari la shule waliokuwemo kuangukia kwenye korongo lililojaa maji eneo la Dampo mkoani Arusha, saa 12 asubuhi ya leo April 12, 2024.
Akithibitisha tukio hilo, Kamanda wa Jeshi la Zimamoto Mkoa wa Arusha, Osward Mwanjejele amesema gari hilo lilitumbukia kwenye korongo linalomwaga maji yake katika mto mkubwa wa Themi.
"Kwa taarifa za awali zinasema kuwa gari lilikuwa na wanafunzi 11 na walimu wawili na dereva na hapo hapo walisaidiwa wanafunzi wanne,mwalimu na dereva," amesema.
Mashuhuda wa ajali hiyo, Evance Rafaeli amesema gari hilo linapita kila siku asubuhi kuchukua wanafunzi katika kaya mbalimbalikuwapeleka shule, lilipita asubuhi kufuata wanafunzi, lakini wakati linarudi lilikuta maji yamejaa na kutokea ajali hiyo.
"Tulisikia kelele za mama mmoja hapa jirani na kijiwe chetu cha kufyatua matofali na katika kukimbia ndio tukaona gari la wanafunzi likielea juu ya maji, akasema alimuonya dereva huyo asipite maji ni mengi, lakini akawa mbishi akajaribu kupita kabla maji hayajamzidi nguvu na gari kuporomokea korongoni,'amesema Rafaeli.
Amesema walianza kazi ya kuokoa na walifanikiwa kutoa watu wawili wazima ambao ni mwalimu na dereva pamoja na wanafunzi watatu wakiwa hai, huku mmoja wa kiume akiwa ameshafariki baada ya gari kujaa maji.
Lilian Mussa amesema alifika eneo la tukio na kukuta kazi ya kuokoa watu likifanywa na watu wawili ambao walilazimika kupiga kelele za kuomba msaada, hivyo watu waliokuwapo barabarani walikwenda kusaidia kabla ya gari kuendelea kusogea na watoto wengine wakionekana kusombwa na maji.
Mmoja wa wananchi walioko kwenye timu ya uokoaji, Elia Mbise amesema wamefanikiwa kuopoa mwili wa mtoto mwingine eneo la Muriet, saa sita mchana kabla ya saa 7:15 kuopoa mwili mwingine eneo la Miongoine.
"Kinachotusaidia ni kufuata nguo ambazo huku korongoni tunapopita tunaziona zimekwama kwenye miti ndio tunaokota, lakini tulipofika eneo la Muriet tuliona pia koti katika kuokota kuvuta ndio tukaona ni mwili tukauchukua," amesema na kuongeza;
"Mbali na hilo pia wamefanikiwa kuupata mwili mwingine eneo la Mirongoine ambazo zote zinapelekwa katika chumba cha kuhifadhi maiti iliyoko katika Hospitali ya Muriet."
Mkuu wa Wilaya ya Arusha, Felician Mtahengerwa amesema ajali imetokana na mvua kubwa iliyonyesha usiku katika maeneo mbalimbali katika jiji la Arusha na kuelekeza maji yake katika njia mbalimbali, ikiwemo katika korongo hilo la Sinoni.
Ametumia nafasi hiyo kuwataka wananchi wa Arusha kuwa watulivu wakati zoezi la uokoaji linaendelea, huku akiwataka wazazi kwenda kutambua miili ya watoto wao inayoendelea kuopolewa bila kutaja idadi.
"Tusiwe wepesi kulia na kuhukumnu wote kuwa wamekufa, tusubiri hadi mwisho kikubwa wengine waende Muriet wakatambue miili ya watoto wao ambao inapatikana," amesema.
Amesema dereva wWa gari hilo amekamatwa na Jeshi la Polisi akiwa katika jaribio la kukimbia kabla hajadhibitiwa na wananchi waliokuwa eneo la tukio.