Rais wa Kenya William Ruto Alhamisi jioni alitangaza kifo cha Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Francis Ogolla, kilichotokana na ajali ya helikopta iliyotokea majira ya alasiri Kaskazini Magharibi mwa nchi.
Akihutubia wanahabari katika ikulu ya Nairobi, Ruto alisema kuwa ndege hiyo ya kijeshi ilianguka eneo la Sindar kaunti ya Elgeyo Marakwet mwendo wa saa nane na dakika 20 alasiri.
Ruto alisema watu wengine 9 pia walifariki katika ajali hiyo na kuongeza kwamba maafisa wengine wawili waliokuwa kwenye ndege hiyo walinusurika na wanaendelea kupatiwa matibabu hospitalini.
Tisa hao ni pamoja na Brigedia Swale Saidi, Kanali Duncan Keittany, Luteni Kanali David Sawe, Meja George Benson Magondu, Kapteni Sora Mohamed, Kapteni Hillary Litali, Sajenti Mwandamizi John Kinyua Mureithi, Sajenti Cliphonce Omondi, na Sajenti Rose Nyawira.
"Nina huzuni kubwa kutangaza kwamba Jenerali Francis Omondi Ogolla, Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi ya Kenya, amefariki” Rais Ruto alisema.
Katika taarifa yake, Ruto alisema Ogolla aliondoka Nairobi Alhamisi asubuhi kuelekea kazini katika eneo la Bonde la Ufa, ambako alikagua ukarabati wa shule tano Elgeyo Marakwet.
Pia alikuwa Turkana ambapo alikutana na kuzungumza na wanajeshi waliotumwa huko kabla ya kwenda Pokot Magharibi. Wakati wa ajali hii, Jenerali Ogolla na timu yake walikuwa wakielekea Kaunti ya Uasin Gishu.
Kufuatia kifo cha Ogolla, Ruto ametangaza siku tatu za maombolezo huku bendera zikipepea nusu mlingoti.
"Wakati huu wa maombolezo ya kitaifa, bendera ya Kenya, Bendera ya Jeshi la Ulinzi la Kenya, na bendera ya jumuiya ya Afrika Mashariki zitapepea nusu mlingoti katika balozi za Jamhuri ya Kenya na Kenya nje ya nchi," Ruto alisema.
Uchunguzi umeanza kubaini kilichosababisha ajali hiyo.