Picha hii ya Benchikha inatuma ujumbe gani Msimbazi?

 

ABSA Bank Vacancy - Lead Generator – Tanga Branch

Ni jambo ambalo huwa nadra kutokea katika ligi yetu lakini juzi katika Uwanja wa Liti, Singida tumelishuhudia.


Baada ya mechi ya Simba dhidi ya Ihefu SC kumalizika kwa sare ya bao 1-1, Kocha Abdelhak Benchikha wa Simba akaonekana akiwa amebakia kwenye benchi huku timu zikiwa zimeshatoka uwanjani.


Wachezaji walishakimbilia vyumbani pamoja na maofisa wengine wa benchi la ufundi, mashabiki walikuwa wameshaanza kuondoka uwanjani lakini Benchikha aliamua kubaki mwenyewe katika benchi akionekana ni mwingi wa mawazo.


Kabla ya hapo wakati mchezo unaendelea, Benchikha alitengeneza tukio ambalo sasa limekuwa likisambaa katika mitandao ya kijamii la kuvua kofia yake kwa hasira baada ya mshambuliaji wake, Fredy Michael kukosa bao la wazi ambalo lingeweza kuamua ushindi wa Simba katika mchezo huo.


Kitendo cha Benchikha kubaki uwanjani baada ya mchezo dhidi ya Ihefu SC kinatoa tafsiri nyingi ambazo Simba wanapaswa kuzitafakari na kuzitafutia suluhu kabla mambo hayajaharibika.


Unaweza kuona kama Benchikha anachoshwa na kile ambacho wachezaji wake wanakifanya ndani ya uwanja. Wachezaji wa Simba hawaonekani kama wanajutia kwa timu kuwa na mwendo wa kusuasua na mara kwa mara tumekuwa tukishuhudia wengi wakirudia makosa yaleyale yanayoigharimu timu.


Kocha hawezi kuingia uwanjani kufunga mabao ya wazi ambayo kina Fredy na Jobe wanayakosa wala hawezi kuingia kurekebisha makosa ya kizembe ambayo safu yake ya ulinzi imekuwa ikiyafanya.


Tafsiri nyingine ni kukata tamaa kwa Benchikha katika ndoto zake za kutimiza angalau nusu ya kile ambacho alikiota wakati anaingia mkataba wa kuinoa timu hiyo.


Miongoni mwa malengo ilikuwa ni kuingia nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu ambalo halijatimia baada ya kutolewa na Al Ahly kwenye robo fainali.


Timu yake imetolewa katika hatua ya 16 bora ya Kombe la Shirikisho Tanzania na sasa imeachwa kwa pointi sita na Yanga kwenye Ligi Kuu ambazo zinaweza kuongezeka kufikia tisa ikiwa wapinzani wao hao watashinda leo dhidi ya Singida Fountain Gate.


Lakini pengine Benchikha anawafikiria mashabiki wa Simba ambao anaona hawastahili kupata hiki wanachopitia hivi sasa kutokana na jinsi ambavyo wamekuwa wakiipa sapoti kubwa ndani na nje ya uwanja wake wa nyumbani.


Kuna mashabiki ambao wamepoteza uhai na viungo vyao kwa ajili ya kuisapoti Simba na bado hawaachi kufanya hivyo. Wapo wanaopoteza fedha na mali zao kuifuata popote ilipo lakini sasa hivi hawaonji raha ya kile wanachokigharImia.


Pengine Benchikha anaona kama kikosi chake hakirudishi thamani ya kile ambacho mashabiki wanaipa hivyo sio jambo la kushangaza kuona akibaki mwenye mawazo katika benchi la uwanja wa Liti.


Kuna mengi yapo ndani ya kichwa chake, picha inatosha kuyaelezea.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad