Licha ya mazoea yaliyopo ya ripoti za makocha kutolewa mwishoni mwa msimu kwa upande wa Yanga mambo ni tofauti baada ya kocha mkuu wa timu hiyo, Miguel Gamondi kuwasilisha mapema ripoti kwa mabosi wa klabu hiyo ikiwa ni mikakati ya kuanza kukisuka upya kikosi cha msimu ujao.
Hesabu za Gamondi ambaye jioni ya jana alikuwa uwanjani kuiongoza timu hiyo dhidi ya Singida Fountain Gate katika mechi ya Ligi Kuu Bara ni kuhakikisha anakuwa na kikosi imara zaidi kuliko alichonacho sasa na tayari mabosi wa klabu hiyo wameanza kuipitia na kufanyia kazi mapendekezo aliyoyatoa kwao mapemaaa.
Mabosi wa Yanga akili zao kwa sasa zimegawanyika, kuna upande unasimamia namna gani watamaliza mechi za Ligi Kuu na Kombe la Shirikisho (FA), lakini upande mwingine umeanza kuangalia namna ya maboresho zaidi ya kikosi hicho kutokana na mapendekezo ya Gamondi.
Utakapoongea na mabosi wa Yanga kuhusu zuio la usajili lililotolewa na Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa)na lile la Tanzania (TFF) watakujibu kwamba ‘tutamalizana nao tu, baada ya kuwapa taarifa wanayoitaka’, kisha baada ya hapo wanaendelea na majukumu yao kama kawaida.
Mabosi hao wameshapokea ripoti ya awali ya usajili kutoka kwa benchi la ufundi chini ya kocha huyo raia wa Argentina inayotaka mashine mpya tano kwa msimu ujao na kushtua kwa kubariki baadhi ya wachezaji kufyekwa.
Taarifa kutoka ndani Yanga ni kwamba ripoti hiyo imeonyesha itahitaji kuongeza kipa mmoja atakayechukua moja ya nafasi ya makipa watatu waliopo sasa akiwamo Djigui Diarra, Metacha Mnata na Aboutwalib Mshery. Mmoja kati ya hawa atapewa mkono wa kwaheri.
Kwenye ukuta hasa eneo la mabeki ripoti hiyo imeonyesha kuhitaji beki mmoja wa kushoto ambapo hapa kuna uwezekano mkubwa kwa mkongwe Joyce Lomalisa akapewa mkono wa kwaheri kwani mkataba wake unamalizika mwisho wa msimu huu.
Taarifa zaidi zinasema kuwa, kwa sasa Yanga bado inaendelea na mazungumzo na mabosi wa Singida Fountain Gate juu ya kurefusha mkataba wa beki wa kushoto Nickson Kibabage anayeitumikia Yanga kwa mkopo ambapo benchi la ufundi la Yanga limeonyesha mahitaji ya kuendelea naye.
Ripoti hiyo, inaelezwa pia inahitaji kiungo mkabaji mwenye ubora zaidi au sawa na Khalid Aucho atakayejiunga kikosini kusaidiana na Mganda huyo pamoja na Jonas Mkude aliyepindua meza kibabe kwa kubakishwa baada ya kuonyesha kiwango kikubwa kwenye mechi mbili dhidi ya Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini.
Gamondi pia inaelezwa anahitaji winga mmoja na mshambuliaji wa maana watakaokuja kuongeza nguvu kwenye eneo la mwisho ambalo bado mshambuliaji Joseph Guede ameanza cheche akifunga jana dhidi ya Singida Fountain Gate.
Kwenye wingi kuna Skudu Makudubela, Denis Nkane ambao wamekosa namba.