BAADA ya taarifa za nahodha wa Singida Fountain Gate, Beno Kakolanya kutoweka kambini saa chache kabla ya mchezo dhidi ya Yanga katika Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza, hatimaye uongozi wa timu hiyo umetoa msimamo na kueleza kilichojificha nyuma yake.
Kakolanya ambaye ni kipa namba moja wa timu hiyo amedaiwa kutoweka kambini kabla ya mchezo huo ambao umechezwa leo Aprili 14, 2024 saa 10 jioni na Singida Fountain Gate kupoteza kwa mabao 3-0.
Baada ya mchezo huo, Mwananchi Digital imezungumza na Ofisa Habari wa Singida Fountain Gate, Hussein Massanza ambaye amesema mchezaji huyo aliomba ruhusa ya kutoka kambini kwa meneja wa timu ambaye kwa mujibu wa taratibu za klabu hiyo hana mamlaka ya mwisho ya kutoa ruhusa kwa wachezaji.
Amesema baada ya uongozi wa juu kupata taarifa za ruhusa hiyo iligoma kumruhusu kutoka kambini ikimtaka asubiri mchezo huo umalizike ndipo aondoke, lakini akaamua kuondoka jambo ambalo limewakasirisha waajiri wake.
“Ukiondoka kwenye timu bila ruhusa wewe ni mtoro kwahiyo hatua za kinidhamu zitachukuliwa ili liwe funzo na tunaendelea kuchunguza tuhuma zinazomkabili na uongozi utatoa taarifa baadaye ya zaidi ya jambo hili,” amesema Massanza
Ofisa huyo amedai mchezaji huyo amekuwa na kawaida ya matukio yanayoonekana ni ya kutaka kuihujumu timu kwa makusudi kwani hata mchezo wa mzunguko wa pili ugenini dhidi ya Simba hakucheza baada ya ‘kujivunja’.
“Wachezaji waheshimu timu na waheshimu mikataba yao. Lazima uongozi uchukue hatua kali kuonyesha kwamba hakuna mtu mkubwa kuliko timu,” amesema Massanza
Kocha Msaidizi wa timu hiyo, Ngawina Ngawina akizungumza baada ya kipigo cha Yanga amesema kutokuwepo kwa nahodha wake na wachezaji wengine siyo sababu ya kupoteza mchezo huo, huku akigoma kuzungumzia sakata la kipa huyo akidai liko ngazi za juu kwa viongozi.
“Hii haiwezi kuwa sababu ya sisi kupoteza mchezo wa leo tunawaheshimu Yanga na tumepokea matokeo, suala la Beno Kakolanya kutoweka kambini hilo siwezi kusema chochote liko ndani ya uongozi,” amesema Ngawina
Taarifa ya awali ya klabu hiyo imenukuliwa ikisema “Klabu ya Singida Fountain Gate inasikitishwa na kitendo cha mchezaji wetu, Beno Kakolanya kutoka kambini tukiwa tunakabiliwa na mchezo muhimu kabisa dhidi ya Yanga leo,”
“Kitendo hiki kinaleta maswali mengi hasa ukizingatia kuwa Beno ni mchezaji mzoefu na mmoja wa wachezaji wa kutumainiwa wa timu ya taifa. Tunaendelea kufuatilia taarifa zake na wachezaji wengine wowote ambao wataonekana kuhujumu timu yetu kwenye mechi ya leo na nyingine zinazofuata,” imesema taarifa hiyo.