Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Dkt. Selemani Jafo amesema Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) kwa kushirikiana na Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania lilifanya tathmini kuhusu maporomoko ya tope yaliyotokea mjini Katesh wilayani Hanang mkoani Manyara na kubaini kuwa jiolojia ya Mlima Hanang imeundwa na mwamba dhaifu ambao ulizidiwa na mvua nyingi zilizonyesha kwa kipindi kifupi na kusababisha maporomoko ya tope, miti na mawe.
“Vilevile, tathmini imebaini kuwa shughuli 64 za kibinadamu zisizo endelevu zinazofanyika pembezoni mwa mlima huo zimechangia uharibifu wa uoto wa asili na hivyo kuongeza urahisi wa maporomoko kutokea katika mlima huo.”
Waziri Jafo amesema hayo Bungeni jijini Dodoma wakati akisoma hotuba ya Bajeti ya Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) kwa mwaka wa fedha 2024/2025.