Simba na Yanga |
Jumamosi ya wiki hii, kuna Kariakoo Dabi inapigwa kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam, Yanga ni wenyeji wa mchezo huo wa Ligi Kuu Bara wakiikaribisha Simba.
Hii ni Kariakoo Dabi ya 112 ndani ya Ligi Kuu, huku tukiwa na kumbukumbu ya ile ya mzunguko wa kwanza, waliokuwa wageni, Yanga waliibuka na ushindi mnono wa mabao 5-1 dhidi ya wenyeji wao, Simba.
Ile Kariakoo Dabi ya mzunguko wa kwanza ambayo Yanga waliondoka kifua mbele na mashabiki wao mtaani kutamba sana, inaendelea kuwapa jeuri kuelekea mchezo wa Jumamosi.
Lakini rekodi za hivi karibuni, zinaufanya mchezo huu kuwa wa tofauti na wengi wanavyofikiria, lakini kuna mtu anaweza kunasa kwenye mtego.
Kiuhalisia hivi sasa Yanga ipo katika wakati mzuri, imekuwa ikifanya vizuri kwenye mechi zake huku ikiwa ndiyo kinara wa Ligi Kuu Bara. Simba inashika nafasi ya tatu, tofauti yao na Yanga ni pointi tisa.
Kutokana na mwendo wa timu hizo mbili msimu huu hasa kwa matokeo ya karibuni, wengi wanaipa nafasi kubwa Yanga kufanya vizuri mbele ya Simba, lakini kuna rekodi zinaweza kuamua jambo.
REKODI ZINASEMAJE?
Licha ya kwamba mchezo wa soka wakati mwingine huwezi kutabiri matokeo kwa kuangalia rekodi, lakini hizo zinaweza kutumika kupata taswira ya mchezo utakuwaje.
Rekodi zinaonesha kwamba, katika misimu kumi iliyopita tangu 2013/14, imekuwa ngumu kwa timu moja kupata ushindi ugenini na nyumbani kwenye mechi ya Kariakoo Dabi.
Katika misimu hiyo ambayo zimechezwa mechi 20 za Ligi Kuu zilizohusisha Simba na Yanga, imetokea msimu mmoja pekee timu moja kushinda ugenini na nyumbani. Hiyo ilikuwa katika msimu wa 2015/16 ambapo Yanga ndiyo ilifanya balaa.
Mchezo wa mzunguko wa kwanza uliochezwa Septemba 26, 2015, Yanga wakiwa wageni, walishinda kwa mabao 2-0, wafungaji ni Amissi Tambwe dakika ya 44 na Malimi Busungu dakika ya 79.
Zilipokutana mzunguko wa pili katika msimu huo wa 2015/16, Yanga ikashinda tena 2-0 kwa mabao ya Donald Ngoma (dk 39) na Amissi Tambwe (dk 72). Mechi ilipigwa Februari 20, 2016.
Je rekodi hiyo ambayo Yanga wanaishikilia, wataweza kuirudia msimu huu kwa kushinda mechi zote mbili baada ya ile ya kwanza kumchapa Mnyama 5-1? Tusubiri tuone.
Ukiangalia kilichotokea msimu wa 2015/16, kama kinafanana na ilivyo msimu huu kutokana na wageni ambao ni Yanga, kushinda mechi ya kwanza, huku ile ya pili wao wakiwa wenyeji.
Katika misimu kumi iliyopita zilipokutana timu hizo ndani ya Ligi Kuu, mechi za mzunguko wa kwanza mara nyingi huwa ni sare, lakini zile za mzunguko wa pili ndiyo anapatikana mshindi.
Lakini msimu wa 2015/16, rekodi mpya ikawekwa kwa Yanga kushinda mechi ya mzunguko wa kwanza, kisha ikashinda tena mzunguko wa pili.
Hapo ndipo ulipo mtego wa mchezo wa Jumamosi kwamba, Yanga baada ya kushinda mechi ya mzunguko wa kwanza wakiwa wageni, sasa wapo nyumbani, nini kitatokea?
Imeshuhudiwa ni misimu miwili pekee timu hizo kushindwa kumpata mbabe, ilikuwa 2013/14 na 2021/22, lakini misimu mingine, mzunguko wa kwanza ni sare, mzunguko wa pili mshindi anapatikana.