Uteuzi wa PAUL Makonda Waibua Gumzo Mtandaoni

 

Uteuzi wa PAUL Makonda Waibua Gumzo Mtandaoni

Uteuzi wa Paul Makonda kuwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha umeibua gumzo mitandaoni ambapo watu wametofautiana mtazamo kuhusu uteuzi huo, huku wengine wakieleza amepelekwa Arusha kimkakati.


Jana, Machi 30, 2024, Rais Samia Suluhu Hassan alifanya uteuzi wa viongozi mbalimbali ambapo Makonda aliyekuwa Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM, ameteuliwa kuwa mkuu wa mkoa wa Arusha akichukua nafasi ya John Mongella ambaye atapangiwa kazi nyingine.


Makonda aliteuliwa kuwa Katibu Mwenezi wa CCM Oktoba 22, 2023 baada ya kuwa nje ya ulingo wa siasa kwa takribani miaka mitatu. Amefanya kazi hiyo ya msemaji wa chama kwa miezi mitano pekee.


Uteuzi huo wa Makonda ambaye baada ya kuteuliwa alikuwa mwiba mkali kwa mawaziri na watendaji wa Serikali kupitia ziara zake, umeibua mjadala mitandaoni huku kila mtu akitoa maoni yake kwa namna alivyoupokea uteuzi huo.


Wakili wa kujitegemea, Peter Madeleka ameandika katika ukurasa wake wa X (zamani Twitter) huku akiambatanisha na kipande cha video akieleza kwamba Makonda hakuwa na mamlaka yoyote ya kutoa maagizo kwa mawaziri.


“Ninao wajibu wa kumfundisha Paul Makonda somo la Katiba na sheria na hasa kuhusu haki za binadamu. nadhani, atafaulu tu,” ameandika Madeleka kwenye ukurasa wake wa X baada ya mabadiliko yaliyofanywa na Rais Samia.


Akiwa na mtazamo tofauti, Tobadi Kayusi ameandika: “Hivi malalamiko yanasaidia vipi kukiimarisha chama??? Kwanini tusijikite kwenye hoja za msingi kukifanya chama kuwa vizuri zaidi kuliko kuendeleza taarabu kulingana na teuzi za watawala?”


Kada wa Chadema, Mdude Nyagali ameandika: “Makonda aliteuliwa kuwa mwenezi siku ya hukumu ya kesi ya bandari kwa lengo la kuhamisha agenda ya hukumu ya bandari. Kwa bahati mbaya agenda haikuhama moto uliwaka mpaka Samia akaona atupe kesi ya uhaini. Leo tena Makonda kateuliwa kuwa RC kukiwa na mjadala ya ripoti ya CAG.”

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad