Wabunge Wacharuka Magari ya Serikali Kuwepo Maeneo ya Starehe

 

Wabunge Wacharuka Magari ya Serikali Kuwepo Maeneo ya Starehe

Sakata la magari ya Serikali ya Tanzania kuonekana maeneo ya starehe limewaibua wabunge wakitaka Serikali ieleze mkakati wa kuzuia hali hiyo kwa sababu yamekuwa kero kwa wananchi.


Wabunge hao ni Noah Saputu (Arumeru Magharibi), Festo Sanga (Makete) na Abbas Tarimba (Kinondoni), wamezungumzia suala hilo kipindi cha maswali na majibu bungeni leo Jumatatu Aprili 8, 2024.


Katika swali la msingi, Saputu amehoji ni lini Serikali itazuia kupaki magari ya Serikali sehemu za starehe baada ya saa za kazi.


Akijibu swali hilo, Naibu Waziri wa Ujenzi, Godfrey Kasekenya amesema Serikali kupitia Waraka wa Rais namba moja wa Mwaka 1998 kuhusu hatua za kubana matumizi ya Serikali, ilielekezwa magari yote ya Serikali yanatakiwa kuwa yameegeshwa sehemu zilizotengwa kwa ajili hiyo ifikapo saa 12.00 jioni bila kukosa.


Naibu Waziri wa Ujenzi, Godfrey Kasekenya akizungumza wakati akijibu maswali ya wabunge leo Jumatatu, Aprili 8, 2024. Picha na Merciful Munuo


Amesema waraka huo ulielekeza vinginevyo kuwepo kibali rasmi kinachoruhusu gari la Serikali kuwepo barabarani baada saa 12.00 jioni.


Amesema pia Serikali kupitia Kanuni J.21 ya Kanuni za Kudumu za Utumishi wa Umma za Mwaka 2009 imezuia watumishi wa umma kutumia magari ya Serikali kwa matumizi binafsi.


Hivyo, amesema mtumishi anayekwenda kinyume na maelekezo hayo anatakiwa kuchukuliwa hatua kali za kinidhamu.


“Kwa fursa hii naomba kuwakumbusha maofisa masuuli wote kusimamia maelekezo hayo,” amesema.


Katika swali la nyongeza, Sanga amesema licha ya sheria kuzuia, lakini bado kwenye baa na maeneo mengine ya starehe magari ya Serikali yamekuwa yakionekana nyakati za usiku.


“Upi mkakati wa makusudi wa Serikali wa kuhakikisha unazuia kabisa kuwepo kwa magari hayo maeneo hayo kwa sababu yamegeuka ni kero kwa wananchi na inaonyesha ni matumizi mabaya ya fedha za Serikali,” amehoji.


Pia, amesema Waziri wa Fedha, Dk Mwigulu Nchemba katika bajeti ya Serikali ya mwaka 2022/2023 amesema Serikali ina mpango wa kuanza kupunguza magari serikalini na watumishi wa Serikali waanze kujinunulia magari kupitia mkopo.


Amehoji ni hatua gani zimechukuliwa hadi sasa, ili kupunguza matumizi ya Serikali kama ilivyotuambia.


Akijibu swali hilo, Kasekenya amewakumbusha na kuwasisitiza maofisa masuuli na waajiri wote kusimamia sheria, kanuni na taratibu zinazoelekeza mtumishi yoyote ambaye ana chombo cha umma asiwe barabarani baada ya saa 12 jioni na kuchukua hatua kwa watakaokwenda kinyume.


“Nadhani wakati Waziri wa Fedha anawasilisha bajeti atalifafanua vizuri kitu gani na wapi Serikali imefanya na inategemea kufanya,” amesema Kasekenya wakati akijibu swali la kuwakopesha magari watumishi.


Naye Tarimba amesema kwa kuwa Serikali imeliambia Bunge zipo sheria na kanuni za kukataza magari ya Serikali baada ya muda wa kazi, Serikali ipo tayari sasa kutoa maelekezo kwa wanaosimamia usalama wa barabarani kuyakamata magari ambayo yanaendelea kukaidi amri hii?


Akijibu swali hilo, Kasekenya amesema sheria zipo na kila chombo kimepewa majukumu yake ya nini kinatakiwa ifanye, nani anatakiwa aione gari iko wapi na nini akifanye wakati gari isipokuwa na kibali cha kuwepo hapo kwa wakati huo.


Amesisitiza vyombo vinavyowajibika kuchukua hatua wanapoona suala hilo.


Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad