Waziri wa TAMISEMI, Mohamed Mchengerwa ametoa pole kwa Wananchi wote walioathiriwa na mvua zinazoendelea kunyesha katika maeneo mbalimbali Nchini ambapo amewalekeza Wakuu wa Mikoa kuhakikisha taarifa za hali ya hewa za kila siku inawafikia Wananchi kwa wakati mpaka ngazi ya Kitongoji ili waweze kuchukua tahadhari hususani katika msimu huu wa mvua zinazonyesha juu ya wastani.
Mchengerwa ameagiza pia Viongozi wote kwenye Sekretarieti za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa kutoa maelekezo na miongozo kwa Wananchi hususani wale wanaoishi kwenye maeneo yaliyoathiriwa na mvua ili kuchukua tahadhari zote za kiusalama.
Pia ameagiza Viongozi wahamasishe Wazazi/Walezi kuwa makini na kuchukua tahadhari za kiusalama kwa Watoto/Wanafunzi wanaokwenda na kurudi kutoka Shuleni hususani kwenye maeneo yalitoathiriwa na mvua.
Mchengerwa amesema Ofisi ya Rais-TAMISEMI inaendelea kufanya jitihada za kuhakikisha kuwa mundombinu muhimu iliyoathiriwa na mvua inarejeshwa ili Wananchi waweze kuendelea na shughuli zao za kila siku.