Mmoja wa wanamuziki maarufu wa nyimbo za Injili Afrika Mashariki, Christina Shusho, amezua mjadala nchini Kenya baada ya kuachia kionjo cha wimbo wake mpya kwa jina Zakayo.
Baadhi ya Wakenya, ambako mwimbaji huyo wa Tanzania ana wafuasi wengi, wamehisi kwamba wimbo huo unamhusu Rais wa Kenya, William Ruto.
Baadhi ya Wakenya kwa dhihaka humtaja Rais Ruto kama Zakayo - Kiswahili kwa mtu anayetajwa katika Biblia, ambaye anajulikana kuwa mtoza ushuru aliyepanda juu ya mti ili kumwona Yesu.
Kwa Kiswahili, Shusho anaimba, "Kulikuwa na mtu mmoja jina lake Zakayo, mkuu wa watoza ushuru na tajiri, alitafuta kuona Yesu ni mtu wa aina gani...
"Bw Ruto alipata jina la utani Zakayo kwa sababu ameanzisha mikakati mingi ya kutoza ushuru mpya, tangu achaguliwe rais mnamo Agosti 2022.
Hilo limemfanya kutopendwa na Wakenya wengi wanaoamini kuwa amesaliti ahadi yake ya kampeni ya kutetea masilahi ya "hustlers" – Wakenya walio wanyonge kifedha .