Meneja wa Young Africans SC, Walter Harson, amezungumzia maandalizi ya mchezo wao wa leo Jumatano dhidi ya Dodoma Jiji.
Mchezo huo wa hatua ya 16 bora ya Kombe la Shirikisho la CRDB Bank, unatarajiwa kuchezwa kwenye Uwanja wa Jamhuri, Dodoma kuanzia saa 2:00 usiku.
Rekodi zinaonesha kwamba, timu ya Young Africans tangu ipoteze kwa goli 1-0 Julai 25, 2021, imefanikiwa kucheza michezo 14 mfululizo ya michuano hiyo bila ya kupoteza, huku ikibeba ubingwa wake mara mbili mfululizo, msimu wa 2021-2022 na 2022-2023.
“Wananchi waelewe kikubwa timu yao imerudi salama kutoka Afrika Kusini, baada ya hapo timu imeunganisha kuja Dodoma kwenye mchezo huu ambao ni muhimu kabisa sehemu ya hatua moja kwenda kwenye malengo ambayo tumejiwekea kama ambavyo unajua.
“Baada ya kutolewa kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika, tumerejea nyumbani kuhakikisha tunafikia malengo ya kuweza kutetea kombe letu kwa maana ya CRDB Federation Cup, lakini pia Ligi Kuu ya Tanzania.
“Hatua hiyo ya kutetea taji hilo inaanzia hapa hatua ya 16 bora dhidi ya Dodoma Jiji, kama ambavyo unajua, Dodoma Jiji ni timu ngumu, timu nzuri yenye benchi la Ufundi bora na wachezaji wazuri na hata katika mchezo wetu wa mzunguko wa kwanza wa ligi pale Chamazi nadhani kila mmoja anajua nini kilitokea.
“Hivyo tumekuja tukiwa na tahadhari ya mambo yote ambayo tunayafahamu kuhusu Dodoma na mwisho wa siku tukiwa tunajiandaa vizuri zaidi ili kuhakikisha tunapata matokeo dhidi ya Dodoma hapo Kesho.
“Hatua hii ya 16, kama kumbukumbu yako ipo vizuri, katika timu 16, moja tu Rhino Rangers iliyocheza dhidi ya Geita ndiyo ilikuwa pekee timu ambayo haikuwa ya Ligi Kuu, hii inakuonesha ubora wa timu ambazo tayari zimefika kwenye hatua hii.
“Kwetu tunaamini unakwenda kuwa mchezo mgumu kwa sababu ya ubora wa Dodoma na ubora wa benchi lao la ufundi chini ya Kocha Baraza na fomesheni wanayocheza.
“Tunaamini hautakuwa mchezo rahisi, utaenda kuwa mchezo mgumu, sisi tumejiandaa na kila hali ambayo tunakwenda kukabiliana nayo katika mchezo na mwisho wa siku tunashinda na kwenda hatua inayofuata.
“Hatuna sababu nyingine yoyote ambayo itatufanya kushindwa kutimiza malengo yetu, kama unavyojua, matarajio ni makubwa sana kwa mashabiki wa Young Africans kwa maana ya Wananchi.
“Kila kitu ambacho tumekifanya msimu uliopita kama tukishindwa kufanya msimu huu itamaanisha kwamba tumeshuka kiwango, kwa hiyo kwetu sisi ni lazima kuhakikisha tunapata matokeo ambayo yatatupeleka hatua inayofuata ili tuweze kuhakikisha tunatimiza lengo la kutetea kombe letu,” alisema Harson.
NENO KWA WANANCHI
“Mashabiki wa Wananchi kama ambavyo imekuwa kawaida yenu, mmekuwa mkitupa sapoti kubwa sana ndani na nje ya nchi, sasa tupo Dodoma. Mashabiki wa Dodoma na walio karibu kwa maana ya Iringa, Morogoro, Arusha, kesho ni siku nyingine ambayo tuna nafasi ya kuhakikisha tunakuwa sehemu ya mafanikio ya Young Africans.
“Karibuni sana kwenye Uwanja wa Jamhuri mje kutupa sapoti na tunaamini kabisa tunaenda kwenye hatua ya robo fainali kwa sapoti ambayo itatoka kwenu, karibuni mtupe sapoti na sisi tunaahidi hatutawaangusha.”