Kocha Mkuu wa Namungo FC, Mwinyi Zahera amesema kuwa iwapo mshambuliaji kinda wa Yanga SC, Clement Mzize amepata dili la kwenda Ulaya ni vyema akaenda huko badala ya kwenda Azam FC.
Zahera ambaye alikuwa Mkurugenzi wa Maendeleo Soka la Vijana ndani ya Yanga, ndiye aliushauri uongozi wa Yanga kumpandisha Mzize kutoka timu ya vijana Under 20 kwenda timu kubwa kutokana na uwezo wake.
Kocha huyo ambaye pia aliwahi kuwa Kocha Mkuu wa Klabu ya Yanga, alimshauri Mzize kutokimbilia kwenda Ufaransa na badala yake acheze timu ya wakubwa ili apate uzoefu huku akimtabiria makubwa kuwa huenda akaja kuwa Didier Drogba wa Tanzania siku za usoni.
"Nimesikia kuwa kuna ofa ya Yanga, Azam na nyingine kutoka nje ya Tanzania zinazomhitaji Clement Mzize, nafikiri kwa umri wake kama kweli kuna ofa ya nje basi ili kukua zaidi na kuendelea kujifunza vitu vipya anapaswa kwenda nje," amesema Zahera.
Azam wameshakiri kuwa wametuma ofa Yanga wakimhitaji Mzize huku kukiwa na ofa nyingine ya timu ya Uingereza ya Watford ambayo nayo inaitaka huduma ya kinda huyo aliyeaminiwa na Kocha Miguel Gamondi.