Meneja wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Klabu ya Simba, Ahmed Ally amelitaka Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kuchunguza namna ambavyo wapinzani wao, Yanga SC wamekuwa wakipata matokeo yao.
Ahmed amesema hayo baada ya mchezaji wa Coastla Union, Lameck Elias Lawi kufutiwa kadi nyekundu aliyopewa na mwamuzi Raphael Ikambi wa Morogoro kwa kosa la kumvuta jezi kiungo mshambuliaji wa Yanga, Aziz Ki wakati wa mchezo wa Ligi baada ya kamati kubaini kuwa waamuzi walishindwa kutafsiri kanuni.
“Hii haiwezi kuwa bahati mbaya ndani ya msimu mmoja wachezaji wawili wa timu tofauti wanapewa kadi za uongo dhidi ya timu moja. Tena katika Mazingira ya kufanana pale ambapo mechi inapokua ngumu dhidi yao.
“Zabona Mayombwa wa Prisons alipewa kadi nyekundu ya Uongo dhidi ya Yanga sc, katika mchezo huo matokeo yalikua 2-1 na Zabona alikua tishio dhidi ya wapinzani na angeweza kabisa kuisaidai timu yake kupata ushindi au sare lakini kwa makusudi akapewa kadi nyekundu ili kuidhoofisha Prisons.
“Lameck Lawi wa Coastal kapewa kadi nyekundu ya magumashi dhidi ya timu ile ile na tena katika mazingira yale yale, Mechi ilikua 0- 0 na Lawi aliwadhibiti vilivyo Nyuma Mwiko, Lakini kwa makusudi akaoneshwa kadi nyekundu ili kuidhoofisha Coastal Union.
“Hii haiwezi kuwa bahati hata kidogo. Bodi ya ligi Tanzania mnafanya kazi nzuri sana kuzifuta hizi kadi za dhulma lakini isiiishie hapo kwani timu zinaathirika.
“Chunguzeni zaidi kujua kuna nini nyuma ya pazia kuzifuta kadi tuu haiwezi kuwa tiba ya kudumu ya hii dhulma. Msimu wa juzi kulikua na trend ya kutolewa penati za uongo kumbuka penati ya Namungo dhidi ya Yanga SC pale Ilulu Lindi.
“Kumbuka Penati ya Ruvu Shooting dhidi ya Yanga sc Kirumba Mwanza. Asante ni kwamba Waamuzi wote waliadhibiwa japo tayari timu zimeathirika.
“Hofu yangu ni kuwa inawezekana wamekuja style mpya ya kudhulumu kwa kutumia kadi nyekundu ndio maana naomba Bodi ya ligi ku deal na hii kitu kwa undani ili kukomesha dhulma hii.”