Dodoma. Mwili wa Askofu Mkuu wa Makanisa ya Methodist Tanzania (TMC), Askofu Joseph Bundala (55) amezikwa kwenye kanisa la Methodist lililopo Ihumwa jijini Dodoma bila kupewa heshima za mazishi kama kiongozi mkuu wa kanisa hilo kutokana na kujinyonga hadi kufa kitendo, ambacho kanisa hilo linaamini ni dhambi.
Mazishi hayo yamefanyika leo Jumatatu, Mei 20, 2024 kwenye kanisa la Methodist lililopo Ihumwa jijini Dodoma.
Viongozi wa dini waliofika kwenye ibada ya mazishi wamewataka waumini wa kanisa hilo kuwa na uvumilivu kwenye kipindi hiki cha msiba na kumwachia Mungu kazi ya kuhukumu.
Askofu Bundala alifariki dunia Mei 16, 2024 kwa kujinyonga ofisini kwake, iliyopo kwenye kanisa la Methodist, Mtaa wa Ipagala A jijini Dodoma.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kaimu Kamanda wa Polisi mkoani Dodoma, Alchelaus Mutalemwa, Polisi walikuta nyaraka zilizoonyesha marehemu alijiua, kutokana na madeni aliyokuwa nayo pamoja na mgogoro wa shule binafsi aliyoiuza.
Hata hivyo, ndugu wa marehemu walipozungumza na gazeti hili Jumamosi walisema hawaamini kama amejinyonga na kutaka uchunguzi zaidi.
Kamanda Mutalemwa aliwajibu akisema bado wanaendelea na uchunguzi wa kifo hicho na hakuna mtu anayeshikiliwa.
Leo Jumatatu, Mei 20, 2024 katika mara baada ya mazishi hayo, Makamu Askofu wa kanisa hilo, Samuel Nyanza amesema Askofu Bundala amezikwa kwa kupewa heshima kama binadamu yeyote anayestahili heshima anapozikwa lakini si kama kiongozi mkuu wa kanisa hilo.
Amesema hiyo inatokana na askofu huyo kujinyonga mpaka kufa kitendo ambacho kanisa hilo linaamini kuwa ni dhambi.
Amesema kanisa limefanya ibada ya kawaida ya maziko ya askofu huyo na hakuna liturjia ya kanisa iliyofuatwa.
"Mazingira ya kifo chake ndiyo yaliyosababisha tumzike kikawaida na tumetumia ripoti ya awali ya jeshi la polisi iliyosema Askofu Bundala amejinyonga sasa kama taarifa itakuja tofauti na hii ya awali tutarudia kufuata utaratibu wa liturujia kwa ajili ya kumpa heshima zote," amesema Askofu Nyanza.
Alipoulizwa watarudia kwa utaratibu upi wa kuufukua mwili au la, Nyanza ambaye atakuwa Mkuu wa Kanisa hilo kwa mujibu wa katiba ya kanisa amesema hawatafukua mwili bali watafuata liturujia inavyotaka hasa kwenye suala la kutoa heshima, maombi na ibada maalum ambayo itafanyika kanisani tofauti na jana ambapo ibada ilifanyika nyumbani.
Askofu Nyanza amesema msimamo wa kanisa hilo ni kwamba mtu aliyeua au kujiua mwenyewe ni dhambi.
Awali, akizungumza kwenye ibada hiyo iliyohudhuriwa na waombolezaji wengi wakiwemo viongozi wa madhehebu mbalimbali, viongozi wa serikali na wamiliki wa shule binafsi Mkoa wa Dodoma, Msaidizi wa Askofu kutoka Dayosisi ya Kati, Askofu Daudi Samweli amesema kilichotokea ni uamuzi binafsi ya Askofu Bundala na siyo msimamo wa kanisa.
Amelitaka kanisa lisitetereke katika kipindi hiki cha msiba wala wasirudi nyuma kwani imani ni lazima iendelee kulindwa kwani kilichotokea kimeshatokea na hawawezi kubadilisha matokeo.
"Tumesikitika sana kutokana na tukio hili, lakini tumwachie Mungu ajuaye ndiye atoe hukumu kwa kuwa hakuna mtu asiyekuwa na dhambi na ndiyo maana Yesu alikufa," amesema Askofu Samweli.
Kwa upande wake, Askofu wa Kanisa la Christian Methodist, Fabian Kikopo amesema hakuna sababu ya watu kuhukumu tukio la kifo cha Askofu Bundala, kwani naye alikuwa ni mwanadamu kama walivyo wanadamu wengine na kulitaka kanisa kutokata tamaa Bali wasonge mbele katika imani na msiba huo uwaimarishe zaidi badala ya kuwagawanya.
Naye mwenyekiti mstaafu wa umoja wa makanisa ya Pentecoste Tanzania (CPCT), Askofu Peter Konki, amesema kila mtu ana njia yake ya kwenda mbinguni hivyo linapotokea jambo la mauti ni kweli linaumiza, lakini halina budi kutokea na badala ya kuanza kuhukumu watumie nafasi hiyo kumtafuta Mungu zaidi.
"Hata katika hili bado tunaendelea kuiamini kuwa Mungu atabaki kuwa Mungu, hivyo tusirudi nyuma tuendelee kumwamini Mungu.