AZAM FC imetangulia kwenda fainali ya Kombe la Shirikisho (FA), Yaisubiri Yanga, Ihefu




AZAM FC imetangulia kwenda fainali ya Kombe la Shirikisho (FA) baada ya kuichapa Coastal Union mabao 3-0 kwenye mchezo wa nusu fainali uliopigwa leo Jumamosi kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini hapa ikimsubiri mshindi wa nusu fainali ya pili itakayochezwa kesho Jumapili kati ya Ihefu dhidi ya Yanga.

Mabao yaliyoipeleka Azam FC fainali yalifungwa na Abdul Seleman 'Sopu' aliyepachika mawili kwa mkwaju wa penalti dakika ya 42 baada ya mabeki wa Coastal Union kuunawa mpira wa shuti lililopigwa na Feisal Salum ndani ya eneo lao la hatari, lingine kwa kichwa dakika ya 83 akiunganisha krosi ya Lusajo Mwaikenda.

Lingine lilifungwa na Feisal Salum 'Fei Toto' dakika ya 73 kwa kichwa akiunganisha mpira wa kona iliyochongwa na Sopu na kuwafanya mastaa hao wawili kuhusika kwenye mabao yote matatu.

Azam FC imefuzu fainali hiyo kwa msimu wa pili mfululizo ambapo msimu uliopita ilipoteza kwenye fainali kwa bao 1-0 mbele ya Yanga katika Uwanja wa Mkwakwani, Tanga. Fainali ya msimu huu itachezwa Juni 2.

Hii ni fainali ya nne kwa Azam katika mashindano hayo baada ya kucheza 2015–16, 2018–19 na 2022-23. Msimu wa 2018-19 ilifanikiwa kubeba ubingwa ikiichapa Lipuli FC bao 1-0 kwenye Uwanja wa Ilulu mkoani Lindi.

Fei Toto ameendelea kuwa mwiba mchungu kwa Coastal Union msimu huu ambapo katika mechi tatu walizokutana amefunga mabao matatu akifunga kila mchezo. Alifunga katika mechi mbili za Ligi Kuu Uwanja wa Mkwakwani (1-0) na Chamazi (1-1).

Kwa ushindi huo Azam FC inaendeleza ubabe kwa Coastal Union msimu huu ambapo katika mechi mbili timu hizo zilipokutana kwenye Ligi Kuu Bara, Azam imeshinda bao 1-0 katika Uwanja wa Mkwakwani, Tanga Oktoba 6, 2023 huku mchezo wa pili uliochezwa Azam Complex Machi 6, mwaka huu ukimalizika kwa sare ya 1-1.

Mchezo huo ambao haukuwa na mashabiki wengi waliohudhuria uwanjani, ulianza taratibu kwa timu zote kushambuliana kwa zamu, kushtukiza na kwa tahadhari kubwa ili kutoruhusu bao la mapema.


Coastal Union walikuwa wa kwanza kuijaribu ngome ya Azam FC, katika dakika ya 7 kwa shambulizi kali lakini winga wake, Haji Ugando alishindwa kuuzamisha mpira nyavuni baada ya kumuacha kipa wa Azam, Mohamed Mustapha, shuti lake likatoka nje kidogo ya lango.

Dakika ya 14, Azam FC ikajibu shambulizi hilo kupitia Fei Toto ambaye alifumua shuti kwa mguu wa kushoto likatoka pembeni kidogo ya lango la Coastal Union.

Azam waliendelea kufanya mashambulizi langoni mwa Coastal Union kupitia Kipre Jr, Fei Toto na Gibril Syllah lakini walikosa umakini katika umaliziaji na kushindwa kuifungia mabao timu yao.


Baada ya kipindi cha kwanza Azam FC kwenda mapumziko ikiwa mbele kwa bao 1-0 lililofungwa na Sopu dakika ya 42 kwa mkwaju wa penalti, kipindi cha pili Azam FC ilikuja tofauti ikisahihisha makosa yake kwenye eneo la umaliziaji na kuikamata mazima Coastal Union ikiongeza mabao mawili na kujihakikishia nafasi ya kucheza fainali ya michuano hiyo kwa mara ya pili mfululizo.

Timu zote zilifanya mabadiliko ya wachezaji kipindi cha pili, Azam FC waliwapumzisha James Akaminko, Pascal Msindo, Sopu na Fei Toto, nafasi zao wakaingia Adolf Mtasingwa, Nathaniel Chilambo, Ayoub Lyanga na Iddi Nado dakika ya 70, 81 na 87, huku Coastal wakiwatoa Gerson Gwalala na Crispin Ngushi wakaingia Lucas Kikoti na Salim Aiyee dakika ya 65 na 74.

Azam kikosi kilichoanza leo: Mohamed Mustapha, Lusajo Mwaikenda, Paschal Msindo, Yeison Fuentes, Yanick Bangala, Yahya Bin Zayd, James Akaminko, Abdallah Seleman 'Sopu', Kipre Jr, Feisal Salum, Gibril Syllah.

Coastal Union: Lay Matampi, Jackson Shija, Miraji Zambo, Fely Mulumba, Lameck Lawi, Charles Semfuko, Gerald Gwalala, Haji Ugando, Crispin Ngushi, Bakari Seleman, Roland Beakou.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad