Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA), imetangaza kupanda kwa bei kikomo za bidhaa za mafuta ya petroli hapa Nchini zitakazotumika kuanzia leo Jumatano May 01, 2024 saa 6:01 usiku ambapo kwa mwezi huu wa May 2024, bei za rejareja za mafuta katika Mkoa wa Dar es Salaam petrol ni Tsh. 3314 kwa lita, dizeli Tsh. 3196 na mafuta ya taa 2840.
EWURA imesema kwa mwezi May 2024, mabadiliko ya bei za mafuta yamechangiwa na ongezeko la bei za mafuta yaliyosafishwa katika soko la dunia (FOB) kwa wastani wa asilimia 3.90 kwa mafuta ya petroli na kupungua kwa wastani wa asilimia 1.31 kwa mafuta ya dizeli, kupungua kwa gharama za uagizaji mafuta (premiums) kwa wastani wa asilimia 7.21 kwa petroli na kwa wastani wa asilimia 2.15 kwa dizeli kwa Bandari ya Dar es Salaam, wastani wa asilimia 10.14 kwa petroli na wastani wa asilimia 23.18 kwa dizeli kwa Bandari ya Tanga na wastani wa asilimia 5.32 kwa mafuta ya petroli na dizeli kwa Bandari ya Mtwara.
“Mabadiliko hayo yamechangiwa pia na kubadilika kwa kiwango cha kubadilishia fedha za kigeni (exchange rate) na kuendelea kutumia EURO kulipia mafuta yaliyoagizwa, Wafanyabiashara wa bidhaa za mafuta kwa rejareja wanatakiwa kuuza mafuta kwa
bei zinazooneshwa kwenye jedwali (kwenye swipe)”
Itakumbukwa bei kikomo za bidhaa za mafuta ya petroli hapa nchini kwa mwezi uliopita zilizoanza kutumika kuanzia Jumatano April 03, 2024 saa 6:01, bei za rejareja za mafuta katika Mkoa wa Dar es salaam petrol ilikuwa ni Tsh. 3257 kwa lita, dizeli Tsh. 3210 na mafuta ya taa 2840.