Coastal, Azam Nusu Fainali ya Kibabe la Kombe la Shirikisho Leo

 

Coastal, Azam Nusu Fainali ya Kibabe la Kombe la Shirikisho Leo

Leo mchezo wa nusu fainali ya kwanza Kombe la Shirikisho utachezwa katika Uwanja wa CCM Kirumba, jijini Mwanza kati ya Coastal Union dhidi ya Azam FC, huku vita kubwa ikiwa ni kusaka nafasi ya kucheza Kombe la Shirikisho Afrika msimu ujao.


Azam FC inakamata nafasi ya pili kwenye Ligi Kuu Bara ikiwa na pointi 60 baada ya michezo 27, huku Coastal Union ikiwa nafasi ya nne na alama 38, ambapo Tanzania itawakilishwa na timu nne kwenye michuano ya kimataifa barani Afrika msimu ujao akiwemo bingwa wa Kombe la Shirikisho.


Mchezo huo utakuwa wa tatu kwa Coastal Union na Azam FC kukutana msimu huu na katika mechi mbili za Ligi Kuu Azam imeshinda moja huku mchezo mwingine ukimalizika kwa sare ya 1-1.


Nusu fainali hiyo itachezwa kuanzia saa 9:30 alasiri ambapo mshindi wa mchezo huo atacheza fainali na mshindi wa nusu fainali nyingine kati ya Ihefu na Yanga.


Akizungumzia maandalizi ya mchezo huo, Kocha Mkuu wa Coastal Union, David Ouma, amesema wanakwenda kuikabili timu ambayo iko kwenye fomu na wmendelezo mzuri zaidi msimu huu huku akiamini mtanange utaamuliwa na uwezo wa mchezaji mmoja mmoja.


“Mimi kama Kocha nina uelewa naamini nitafanya kazi nzuri ni mtihani mzuri kwetu dhidi ya Azam ambayo iko kwenye fomu ina wachezaji wazuri wana Feisal Salum ambaye anawania ufungaji bora ni tishio kwetu, mimi pia nina kipa mzuri (Lay Matampi) mpaka sasa ni sare lakini huenda ikaamuliwa na mchezaji mmoja mmoja,” amesema Ouma


“Tutakuja na mpango mzuri kwa kuchagua wachezaji ambao wako fiti na wana morali nzuri ya kucheza mchezo huo, kesho ningependa wachezaji wangu wajitolee wafurahie mpira wapambane ninafahamu Azam ni timu ya namna gani nitapambana kupata mbinu bora zaidi itakayotufanye tupate ushindi.”


Mchezaji wa timu hiyo, Jackson Shija, amesema: “Sisi wachezaji tuko tayari kimwili na kiakili kucheza kesho, ni mechi ngumu tunawaheshimu Azam ni timu bora lakini sisi tuko tayari kupambana na kusonga mbele.”


“Walimu wetu na benchi la ufundi wamesimamia vizuri na kuangalia tulichofanya michezo miwili iliyopita dhidi ya Azam FC, tuwaahidi mashabiki watarajie vitu vingi kesho dhidi ya Azam.”


Kocha wa Azam FC, Bruno Ferry, amesema Coastal Union wanacheza vizuri mpira wa kuzuia hivyo mastaa wake wanapaswa kuwa makini wakati wote, huku beki, Nathaniel Chilambo, wanafahamu hawajafanya vizuri kwenye mashindano yoyote msimu huu hivyo mchezo wa kesho ni muhimu kwao na unawapa hamasa ya kushinda na kwenda fainali.


Ofisa Habari wa Azam, Thabiti Zakaria amesema: “Coastal ni timu nzuri inacheza mchezo mzuri walimu wamefanya kazi yao, kitakacholeta utoafuti ni nguvu ya mashabiki sisi tuna matawi hapa Mwanza na uwanja huu umekuwa mzuri kwetu.


“Ni muhimu sana tukatoa kila nguvu tuliyonao msimu huu, tukisema mchezo huu tutunze silaha tulizonazo tutazitoa mchezo gani, lazima tutoe silaha zetu zote kuhakikisha tunapata ushindi,” amesema Zakaria

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad