MKURUGENZI wa Shirika la Haki, Godlisten Malisa na mwanachama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Boniface Jacob, wamepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam, wakikabiliwa na mashtaka matatu likiwemo la kuchapisha na kusambaza taarifa za uongo mitandaoni. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam…(endelea).
Malisa na Jacob wamepandishwa kizimbani leo Jumatatu, tarehe 6 Mei 2024, ikiwa ni siku chache tangu waachiwe kwa dhamana tarehe 27 Aprili mwaka huu, baada ya kujisalimisha katika Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, tarehe 25 Aprili 2024.
Mashtaka dhidi ya washtakiwa hao wawili yalisomwa mahakamani hapo na mawakili wa Serikali, Happy Mwakamale, akishirikiana na Neema Moshi, mbele ya Haki Mkazi Mkuu, Ushindi Swallo.
Akisoma mashtaka hayo, Wakili Mwakamale amedai Jacob na Malisa wameshtakiwa chini ya kifungu cha 16 cha Sheria ya Makosa ya Kimtandao namba 14 ya 2015.
Katika mashtaka hayo, inadaiwa Jacob kupitia ukurasa wake wa mtandao wa X unaofahamika kwa jina la @ExMayorUbungo, kwa makusudi ya kupotosha umma, alichapisha taarifa za uongo kupitia mfumo wa kompyuta.
Inadaiwa kuwa tarehe 19 Machi 2024, kwa kujua na kwa nia ya kupotosha umma, Jacob pia alichapisha taarifa za uongo kupitia ukurasa wake wa mtandao wa X.
Katika shtaka la tatu linalomhusu mshtakiwa wa pili (Malisa), mnamo tarehe 22 Aprili mwaka huu, kwa kujua na kwa lengo la kupotosha umma alichapisha ujumbe wenye taarifa za uongo, kupitia mtandao wa Instagram wenye jina la Malisa-gj.
Kesi hiyo imeahirishwa hadi tarehe 6 Juni 2024 itakapoitwa kwa ajili ya kusikilizwa, baada ya ahirisho hilo washtakiwa wote wawili wameachiwa kwa dhamana.
Washtakiwa hao kabla ya kupandishwa kizimbani walihojiwa na Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, kwa tuhuma za kutoa taarifa za uongo zilizodai Robert Mushi maarufu kama Babu G, ameuawa chini ya mikono ya polisi na kwamba mwili wake ulihifadhiwa katika Hospitali ya Polisi Kilwa Road, Dar es Salaam.