Imeisha Hiyo, Sancho Kurejea Man United

 

Imeisha Hiyo, Sancho Kurejea Man United

Mabosi wa Manchester United wamesafiri kwenda Ujerumani kukutana na winga wao Jadon Sancho kufanya mazungumzo maalumu yenye lengo la kumshawishi staa huyo wa England arudi Old Trafford msimu ujao.


Sancho, aliyesajiliwa na Man United kwa ada ya Pauni 73 milioni, alirudi Borussia Dortmund kwa uhamisho wa mkopo kwenye dirisha la Januari, mwaka huu baada ya kutibuana na kocha Erik ten Hag.


Siku chache zilizopita kulikuwa na ripoti kwamba Sancho amefuta mpango wa kurudi Man United, hata kama kocha Ten Hag atakuwa ameondoka kwenye timu hiyo baada ya kuona Ujerumani ndipo panapomfaa zaidi.


Lakini, kocha Ten Hag anafichua kwamba kumekuwa na vikao baina ya Sancho na mabosi wa timu hiyo wakijaribu kufuatilia maisha yake ya huko Ujerumani na uwezekano wa kumrudisha kwenye timu.


Ten Hag alisema: “Tupo kwenye michakato. Tumekuwa tukihudhuria mechi ambazo Jadon amekuwa akicheza.


“Tumemtembelea, tumezungumza naye na tutaendelea na mchakato huo.”


Kikao kilichofanyika kiliwahusu mkurugenzi wa soka anayemaliza muda wake Man United, John Murtough na mkurugenzi wa makubaliano ya wachezaji, Matt Hargreaves, ambao walimfuata Sancho huko Ujerumani.


Sancho alitibuana na kocha Ten Hag, Septemba mwaka jana baada ya kuwekwa benchi kwenye mechi ya kipigo kutoka kwa Arsenal katika mchezo wa Ligi Kuu England.


Baada ya mechi hiyo, kocha Ten Hag alielezea kukosakana kwa Sancho ni kwamba hakuonyesha kiwango kizuri mazoezini. Jambo hilo lilimfanya Sancho kujibu kupitia mtandao ya kijamii, alisema kocha wake ni muongo na kwamba anachokifanya ni kumfanya tu kuwa mbuzi wa kafara.


Baadaye, Sancho alifuta posti yake hiyo kwenye mtandao wa kijamii, lakini aligoma kumwomba radhi kocha Ten Hag kwa kile alichofanya kwa kumsema hadharani kwamba ni muongo.


Alipigwa mafuruku kufanya mazoezi na kikosi cha kwanza, akaambiwa akafanye mazoezi kivyake na wachezaji wa kwenye akademia, kabla ya kufunguliwa mlango wa kutokea kwenye dirisha la Januari, alipokwenda kwa mkopo kwenye klabu yake ya zamani ya Borussia Dortmund.


Na tangu alipotua Dortmund, Sancho amecheza kwa kiwango kikubwa sana, hasa kwenye mechi ya kwanza ya hatua ya nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, ambapo chama lake la Dortmund liliibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Paris Saint-Germain.


Na sasa kocha Ten Hag anataka waweke tofauti zao pembeni baada ya msimu huu kumalizika.


Mdachi huyo alisema: “Kulikuwa na mgogoro, lakini kwanza acha tumalize msimu na kisha tutamalizana na ishu hiyo, kwa sasa sio muhimu.


“Ana mechi ya marudiano ya nusu fainali, kwenye ligi hawapo vizuri na sisi tuna mechi zetu za kumalizia pamoja na fainali ya Kombe la FA, baada ya hapo tutajua.”


Ni wazi Ten Hag ameanza kufikiria namna ya kukijenga upya kikosi chake kwa ajili ya msimu ujao, akiamini kwamba ataendelea kuwa kocha kwenye kikosi hicho cha Old Trafford.


Amekiri kwamba anahitaji kuwa na kikosi kipana baada ya msimu huu kuandamwa na majeruhi wengi.


“Moja ya ishu kubwa ni kukijenga kikosi. Tunahitaji kujenga kikosi chetu kuwa bora na kiwe kipana.”


Kwenye hilo la wachezaji, Ten Hag ana mastaa wake anaolenga kuwanasa pia, akisema: “Nadhani kila kocha anahitaji kuwa na wachezaji wenye dhamira ya ushindi. Akili kubwa na uwezo wa kupambana kwenye mazingira yoyote. Kwenye klabu hii ni kitu cha kawaida kucheza kwenye presha kubwa.”


Mchezaji ambaye bila ya shaka Ten Hag atapambana kubaki naye kwenye kikosi ni nahodha Bruno Fernandes, ambaye wiki iliyopita alishtua baada ya kueleza kwamba atafikiria hatima yake kwenye kikosi cha Man United baada ya fainali za Euro 2024.


Kocha Ten Hag alizungumzia ishu hiyo ya Fernandes, akisema: “Hiyo naamini ilieleweka vibaya. Najua yeye ni Manchester United na ana furaha kubwa ya kuwa hapa.”


Ten Hag alisema nahodha huyo ni mchezaji wa mfano kwenye kikosi na kuwapa funzo wale wanaoshindwa kucheza kwa sababu tu wanasumbuliwa na maumivu.


“Bruno ni mpambanaji halisi. Kwa mfano mwaka jana, tulicheza na Brighton kwenye nusu fainali ya Kombe la FA akiwa na maumivu makali kwenye enka. Bruno ni mfano bora kwa wachezaji wengine.”


Man United usiku wa jana Jumatatu ilitarajia kukipiga na Crystal Palace kwenye mchezo wa Ligi Kuu England.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad