Licha ya uongozi wa klabu ya Yanga kutoweka wazi usajili wa winga wa kulia wa TP Mazembe raia wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Phillipe Kizumbi, mchezaji huyo amejitokeza na kuwashukuru mashabiki wa klabu hiyo kwa kumkaribisha na kumfanya aongeze marafiki wengi katika mitandao yake ya kijamii.
Inaelezwa Yanga wameshamalizana na mchezaji huyo na msimu ujao atacheza Ligi Kuu Tanzania Bara akiwa na mabingwa hao.
Nyota huyo ameposti video fupi akiwa amevaa jezi ya Yanga, akiwashukuru mashabiki wa klabu hiyo kuwa sehemu ya familia ya Mabingwa hao.
Mchezaji huyo amesema anafurahi kuona mashabiki wa Yanga wamejitokeza kwa wingi kuungana naye na kumkaribisha kwenye timu yao na kuendelea kuongeza marafiki.
“Nawapenda Yanga wote na nashukuru kwa kuonyesha upendo huu mkubwa, msisahau kunifuatilia najua mnaweza kufanya hivyo jamani, naipenda Tanzania tutaonana hivi karibuni,” amesema nyota huyo kwenye mtandao wake wa kijamii.
Kizumbi amesema anaimani ipo siku atakuja Tanzania lakini hakuweka wazi juu ya timu gani atakuja kucheza na kuwataka mashabiki wake kuvumilia kwa sababu lolote linaweza kutokea katika masuala ya usajili.
Kizumbi ambaye ni mchezaji halali wa TP Mazembe ambayo imeingia makubaliano na Yanga ya kubadilishana wachezaji.
Inaelezwa, Kizumbi atatu Jangwani na mshambuliaji Kennedy Musonda atajiunga na TP Mazembe katika muda wake wa mwaka mmoja uliobaki kwenye mkataba wake.
Mbali na mchezaji huyo tayari Yanga ipo katika mazungumzo na kipa wa Tanzania Prisons, Yona Amos kuchukuwa nafasi ya Metacha Mnata ambaye klabu hiyo ina mpango wa kuachana naye mwishoni mwa msimu.