KOCHA Gamondi Alifagilia Soka la Tanzania, Adai Limekuwa, Atoa Kasoro pia

 
KOCHA Gamondi Alifagilia Soka la Tanzania, Adai Limekuwa, Atoa Kasoro pia


WAKATI Shirikisho la Soka Nchini (TFF), limetangaza rasmi kupeleka Fainali ya Kombe la FA kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar, Kocha Mkuu wa Yanga, Miguel Gamondi, amesema soka la Tanzania limekua ingawa baadhi ya mambo yanatakiwa kufanyiwa maboresho.

"Uamuzi huo umefanywa na Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania baada ya baadhi ya miundombinu muhimu mjini Babati kutokuwa tayari kwa ajili ya fainali hiyo pamoja na sababu za kiusalama.

TFF, imezishauri mamlaka za mikoani Manyara kuendelea kufanya marekebisho katika miundombinu hiyo ili ifikiriwe kwa ajili ya fainali zijazo na michuano mingine mikubwa," ilisema taarifa iliyotolewa na TFF.

Taarifa hiyo iliongeza Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo wa Zanzibar, Tabia Maulid Mwita, atakuwa mgeni rasmi katika fainali hiyo itakayowakutanisha Yanga dhidi ya Azam Juni 2, mwaka huu.

Akizungumza na gazeti hili, Gamondi akiwa na msimu mmoja tu nchini amesema ili Ligi Kuu Tanzania Bara iwe bora zaidi ushindani kutoka katika timu nyingine unatakiwa kuongezeka na kuacha utawala wa timu tatu za Simba, Yanga na Azam.

Gamondi alisema kama hali itabakia hivi ilivyo, vigogo hao watatu watakosa ushindani na badala yake wataendelea kutawala kwa muda mrefu soka la Tanzania.

Alisema pia ili kufanya vizuri kwa timu ambazo zinafundishwa na makocha wazawa, inahitajika walimu hao wazalendo kupatiwa elimu huku nguvu ikiongezwa katika maendeleo ya soka la vijana.

Kocha huyo pia amewapongeza wachezaji wa kigeni kwa kusaidia 'kulichangamsha' soka la Kibongo pamoja na nyota wake kwa ujumla ambao wameonekana kujifunza kutoka kwa wenzao.


"Nchi imepiga hatua kubwa kwa ujumla kwenye soka, lakini bado natatizwa na ushindani kwenye ligi, kwa sababu ni timu tatu tu ndizo zenye ushindani na zenye uwezo mkubwa, kuna utofauti mkubwa kati ya timu tatu za juu na zinazofuata chini ya msimamo, labda ni suala la bajeti, lakini natamani misimu ijayo kuwe na mabadiliko ushindani kutoka katika klabu nyingine, kuwe na uwiano wa ushindani na si hivi," alisema kocha huyo.

Raia huyo wa Argentina pia alionekana kukerwa na baadhi ya viwanja nchini kuwa vinawakwaza makocha wanaofundisha timu mbalimbali zinazoshiriki Ligi Kuu Tanzania Bara.

"Viwanja bado vina changamoto, navyo vifanyiwe kazi, kukiwa na viwanja vizuri kunatoa nafasi kwa wachezaji kucheza vizuri na makocha kufanya kazi kwa uhakika zaidi ikiwamo kupata mafanikio.


Nashauri pia makocha wazawa wapewe elimu ya kuwa makocha wazuri, wapewe nafasi na waaminike kufanya kazi, vile vile kuna tatizo katika utengenezaji wa vipaji vipya katika soka la vijana, bado nguvu iongezeke.

Wachezaji wa kigeni waliopo wamelifanya soka la Tanzania kufahamika na kuheshimika zaidi, lakini wanafanya kazi  kubwa na kuwa chachu ya wazawa kujituma katika vikosi ili kupigania namba, pia hata wachezaji vijana kujifunza kutoka kwao.

Aliongeza wachezaji hao wageni waendelee kuruhusiwa kucheza Ligi Kuu Tanzania Bara kwa sababu uwepo wao 'umenogesha' ligi na kuipa heshima katika ubora wa viwango vya soka Afrika.

Gamondi ataiongoza Yanga katika sherehe za kukabidhiwa kombe la ubingwa Jumamosi baada ya mechi dhidi ya Tabora United itakayochezwa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad