Furaha ya mashabiki wa Simba imerudi upya ndani ya kikosi hicho tangu alipokabidhiwa timu hiyo Kocha Mkuu, Juma Mgunda akichukua nafasi ya Mualgeria, Abdelhak Benchikha aliyeondoka Aprili 28, mwaka huu kutokana na matatizo ya kifamilia.
Simba iliachana na Benchikha ikiwa ni siku moja tu tangu timu hiyo itwae taji la Michuano ya Kombe la Muungano baada ya kuifunga Azam FC bao 1-0, katika mashindano yaliyofanyika na kuhitimishwa rasmi Aprili 27, 2024 huko visiwani Zanzibar.
Wakati mashabiki wa timu hiyo wakiwa wamekosa matumaini kutokana na matokeo mabovu waliyokuwa wanaendelea kuyapata ila ghafla akapatikana mwokozi, Juma Mgunda ambaye tangu akabidhiwe kikosi hicho hadi sasa hajawahi kupoteza mchezo wowote.
Katika michezo minne ya Ligi Kuu Bara ambayo Mgunda ameiongoza Simba kabla ya ule uliopigwa jana dhidi ya Kagera Sugar kwenye Uwanja wa Kaitaba Bukoba, ameshinda mitatu na kutoka sare mmoja tu sawa na kukusanya jumla ya pointi 10 kati ya 12.
Mwenendo huo sio kwamba tu umewafurahisha mashabiki bali hata kwa upande wa viongozi ambao wamepanga kumfanyia sapraizi ya kumwekea mshahara wake mbili zaidi ya huu wa sasa anaolipwa ikiwa timu hiyo itamaliza katika nafasi mbili za juu.
Taarifa ambazo Mwanaspoti imezipata zinaeleza viongozi wa Simba wanamlipa Mgunda Sh11 milioni kwa mwezi hivyo ikiwa timu hiyo itamaliza nafasi ya pili itakayowapa nafasi ya kucheza michezo ya kimataifa msimu ujao wataiongeza mara mbili yaani Sh22 milioni.
“Ni kweli viongozi wamepanga kumuongezea dau zaidi ya hili analolipwa na sababu kubwa ni kumuongezea motisha kutokana na kile ambacho amekifanya ndani ya timu, malengo yetu kwa sasa ni kumaliza tu nafasi ya pili,” kilisema chanzo hicho.
Mwanaspoti liliwatafuta viongozi wa Simba kuzungumzia suala hilo akiwemo ofisa mtendaji mkuu wa timu hiyo, Imani Kajula ambaye hakutoa ushirikiano wowote huku ofisa habari na mawasiliano wa klabu, Ahmed Ally alisema wako bize na mchezo wa jana.
APEWA RUNGU LA USAJILI
Hata hivyo taarifa ambazo Mwanaspoti imezipata zinaeleza Mgunda amepewa uhuru wa kufanyia tathimini kikosi hicho hadi mwisho wa msimu huu wakati huu viongozi wa timu hiyo wakiwa bado wanaendelea na mchakato wa kumpata kocha mwingine mkuu.
Mwanaspoti limepenyezewa taarifa hizo na mmoja wa vigogo wa timu hiyo ambaye aliweka wazi wanatambua na kuthamini kwa kiasi kikubwa mchango wake ndio maana wamempa uhuru huo licha ya viongozi nao kutambua wanapaswa kuanzia maeneo gani.
“Ni kweli amepewa taarifa ya kufanyia tathimini ya kikosi ambayo ataiwasilisha mwisho wa msimu, siwezi kusema moja kwa moja ndiye atakayekuwa kocha mkuu kwa sababu ya mamlaka hayo isipokuwa ni kuthamini anachofanya,” kilisema chanzo hicho.
Hii ni mara ya pili kwa Mgunda kurudi ndani ya timu hiyo kwani mara ya kwanza ilikuwa ni Septemba 7, 2022 alipoachana na Coastal Union na kutua Simba akichukua nafasi iliyoachwa wazi na Mserbia, Zoran Manojlovic Maki aliyeondoka Septemba 6.
Mgunda alidumu ndani ya timu hiyo hadi Januari 3, 2023 kisha kuondoka na nafasi yake kuchukuliwa na Mbrazili, Roberto Oliveira ‘Robertinho’ na katika kipindi chote alikiongoza kikosi hicho katika jumla ya michezo 16 ya Ligi Kuu Bara.
Katika michezo hiyo 16, Mgunda alishinda 11, sare minne na kupoteza mmoja tu ambao ulikuwa kichapo ilichokipata cha bao 1-0, dhidi ya Azam FC lililofungwa na Prince Dube, mechi iliyopigwa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Oktoba 27, 2022.
Mbali na hilo ila aliweka pia rekodi ya kipekee ndani ya timu hiyo ya kuwa kocha mzawa wa kwanza kuifikisha Simba hatua ya Makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika tangu mara ya mwisho alipofanya hivyo, Tito Mwaluvanda akiwa na Yanga mwaka 1998.