Beki wa kati na nahodha wa Klabu ya Yanga, Bakari Nondo Mwamnyeto amekana tetesi zinazosambaa kuwa huenda msimu ujao akaibukia kwa wapinzani wao Simba SC.
Mwamnyeto amesema hayo baada ya Yanga kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya NBC kwa mara ya 30 baada ya kuitungua Mtibwa Sugar mabao 3-1 katika Dimba na Manungu, Turiani mkoani Morogoro.
“Kucheza kwenye kikosi ambacho kina ushindani mkubwa wa namba sikuwa na presha yoyote, nimeshacheza mechi nyingi sana na wachezaji mbalimbali, kikubwa ni umhimu wa mechi kulingana na mwalimu anavyokupanga, akiona mechi hii unafaa kucheza unacheza, Yanga acheze yoyote sisi shida yetu ni alama tatu basi.
“Kuhusu msimu ujao ninawaambia mashabiki kwamba Yanga Bingwa, sina kingine zaidi. Yanayozungumzwa hayanihusu, Yanga Bingwa… Yanga Bingwa… Yanga Bingwa…. Yanga Bingwa. Siondoki Yanga mpaka wanifukuze wenyewe,” amesema Mwamnyeto.
Hivi karibuni kumeibuka tetesi za Yanga kutaka kuachana na beki huyo kwa kile kinachodaiwa kushuka kwa kiwango chake.
Taarifa zinadai kuwa Yanga wanataka kusafisha kikosi chao kwa kuondoa wachezaji wote wasiokuwa na uhakika wa kuanza kikosi cha kwanza cha timu hiyo huku jina la Beki huyo likiwemo.
Wachezaji wengine wanaotajwa kuwemo kwenye mpango wa kupigwa chini Yanga ni pamoja , Kennedy Musonda, Danis Nkane, Zawadi Mauya, Joyce Lomalisa, Metacha Mnata, Skudu na Farid Mussa.