Kuziona Yanga, Ihefu Buku Kumi tu
Wakati homa ya mchezo wa nusu fainali ya pili ya Kombe la FA kati ya Yanga dhidi ya Ihefu FC ikizidi kupanda, kiingilio katika mchezo huo imetajwa ni Sh10,000.
Mchezo huo unaotazamiwa kuwa na upinzani mkali na kusisimua kutokana na ubora wa timu zote, utapigwa katika Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, jijini Arusha na kiingilio cha VIP A na B ni Sh30,000, jukwaa C Sh20,000 huku mzunguko ikiwa Sh10,000.
Jukwaa la VVIP litakuwa ni maalum kwa mwaliko na mashabiki watalazimika kuchagua VIP A, B au C na mzunguko.
Katibu wa Chama cha Soka Mkoa wa Arusha (ARFA), Emmanuel Antony amewahimiza mashabiki kujitokeza mapema kukata tiketi ili kuondoa usumbufu unaweza kujitokeza siku ya mechi.
“Kama ARFA, kwetu ni furaha kuona TFF inatuamini na kutupa mashindano makubwa kama haya, kikubwa tu niwaambie mashabiki wa Yanga na Ihefu wajitokeze kwa wingi kuja kuzisapoti timu zao.”
Yanga imetinga nusu fainali baada ya kuichapa Tabora United mabao 3-0, huku Ihefu ikiichapa Mashujaa FC mabao 4-3 ya mkwaju wa penalti baada ya dakika 90 kukamilika kwa suluhu.
Mshindi kati ya Ihefu na Yanga itacheza fainali dhidi ya mshindi wa nusu fainali ya kwanza itakayopigwa kesho Jumamosi katika uwanja wa CCM Kirumba, jijini Mwanza kati ya Coastal Union FC na Azam FC.
Fainali itapigwa Juni 2 mwaka huu katika uwanja wa Tanzanite Kwaraa uliopo mjini Babati, Mkoa wa Manyara.