Kocha Juma Mgunda |
Kwanini Kocha Mgunda Asiaminiwe na SIMBA moja kwa moja?
Mlete Mgunda. Ni kauli maarufu zaidi kwa wapenzi wa Simba pale mambo yanapokuwa magumu kwao. Kwanini? Subiri nitakwambia.
Hapa majuzi aliyekuwa kocha wa Simba, Abdelhak Benchikha aliomba kuondoka klabuni hapo kutokana na matatizo ya kifamilia.
Ilikuwa ni mshtuko mkubwa sana. Simba ilishaweka matumaini makubwa kwa Benchikha kusuka timu ya msimu ujao.
Benchikha hakua na msimu mzuri sana kwa mwaka huu. Lakini hakukua na lawama kubwa sana kwake kwa kuwa alikuja katikati ya msimu. Akarithi kikosi chenye changamoto nyingi.
Angefanya nini zaidi ya kile? Hakuna. Ndiyo sababu matumaini makubwa kwa Wanasimba yalikua Benchikha apewe wachezaji wa maana kwaajili ya kusuka kikosi cha msimu ujao. Hata hivyo akaondoka kabla ya hilo kutimia.
Viongozi wa Simba wakaanza kuhaha kufikiria mwelekeo mpya. Wampe nani timu? Ni swali gumu. Wakamfikiria Abdihamid Moalin wa KMC. Wakataka wampe kijiti kwa muda.
Ila huko mtaani hisia za mashabiki zilikua tofauti. Wanamtaka Mgunda. Ndiyo mkombozi wao wa nyakati ngumu. Kwanini mashabiki wa Simba wanampenda Mgunda?
Jibu ni rahisi tu. Mgunda aliwapa burudani katika wakati wake. Alipopewa kukaimu nafasi ya Kocha Mkuu mwaka juzi, Simba ilicheza soka la kuvutia. Licha ya kushinda mechi, ila baada ya dakika 90 kila shabiki aliondoka kwa furaha.
Mgunda alishinda mechi nne za awali za kufuzu makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika. Haijawahi kutokea kwa Simba kwa miaka ya karibuni, lakini kwa Mgunda iliwezekana.
Hapa ndipo upendo wa Wanasimba kwa Mgunda ulianzia. Walitamani aendelee kuwa kocha wa kudumu wa Simba kwa wakati ule. Lakini viongozi waliamini tofauti. Waliamini kuwa wanakwenda kwenye mechi ngumu za hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika hivyo walihitaji kocha mwenye wasifu mkubwa zaidi.
Ungewaambia nini viongozi wa Simba wakuelewe? Ni ngumu. Ilikua ni mara ya kwanza kwa Mgunda kuongoza timu kwenye mechi za CAF. Hakua na historia yoyote ya kuwafanya wamwamini Zaidi. Kila kitu kikubwa alichofanya Mgunda, alikifanya akiwa Simba.
Kabla ya kuifundisha Simba, Mgunda amewahi kufundisha timu moja peke yake. Ni Coastal Union ya Tanga. Aliifanya kama familia yake. Aliondoka na kurejea. Kisha akaondoka tena na kurejea. Ndio yalikuwa maisha yake.
Nafasi nyingine kubwa ni kuwa kocha msaidizi wa Taifa Stars. Ndio maeneo ambayo alikuwa amefanya kazi.
Viongozi wa Simba wakaamua kumleta Roberto Oliveira ‘Robertinho’. Huyu alikuwa na mtazamo na falsafa tofauti na ile ya Mgunda. Simba yake haikucheza soka la burudani kama Mgunda, ila ilicheza mpira wa malengo.
Simba ya Robertinho ilijiwekeza zaidi kwenye kushinda mechi na siyo kucheza vizuri. Hapa ndipo mashabiki wa Simba wakaanza kumkumbuka Mgunda. Robertinho aliwarejesha kwenye mpira mgumu. Soka ambayo watu wa Simba hawalipendi.
Miaka yote mashabiki wa Simba wanapenda timu yao ishinde huku ikicheza soka la kuvutia. Ndiyo falsafa ya Simba miaka yote. Aliwahi kufukuzwa Joseph Omog kwasababu hiyo. Simba yake haikuwa inacheza soka la kuvutia sana.
Aliwahi kufukuzwa Dylan Kerr kwa sababu hiyo. Mashabiki walisema timu inashinda ila inakata pumzi katika dakika za mwisho. Wanashinda wakiwa wameshikilia roho. Hayo siyo mambo ya Simba.
Ndiyo maana mashabiki wa Simba kila wakikumbuka namna ‘boli’ lilivyokuwa linatembea wakati wa Mgunda wakatamani arejee tena. Wameona kama viongozi wao wakiendelea kutafuta makocha wa kigeni ni kupoteza fedha wakati Mgunda huyo.
Ila ndio uhalisia. Kwanini Simba wanateseka kutafuta kocha mbali wakati Mgunda akiwa na timu inacheza vizuri. Kwanini hawamwamini wakati walipompa kazi hakufanya vibaya. Alipoteza mchezo mmoja tu katika wakati wake. Alifanya vizuri.
Usishangae akafanya vizuri tena wakati huu amepewa timu na mwisho wa msimu viongozi wakaja na kocha mwingine. Inashangaza sana.
Wakati Simba inacheza fainali ya CAF mwaka 1993, kocha mkuu wa Simba alikuwa Abdallah Kibadeni. Ndiyo mafanikio makubwa zaidi ya Simba kwenye mechi za CAF na waliyapata wakiwa na kocha mzawa lakini sasa wanapata shida sasa kumwamini mwingine.
Wakati huu Simba ikiwa inahaha kusuka kikosi kipya nadhani wangeendelea kuwa na Mgunda. Anaweza kuwaonyesha njia ya kutokea.
Faida kubwa ni kwamba Mgunda ni kipenzi cha mashabiki wao. Wanamuunga mkono kwenye kila hatua. Wanaweza kufanya vizuri zaidi wakiwa na presha ndogo chini ya Mgunda.