Mabaki ya Panya yapatikana kwenye mkate, kampuni yatoa agizo



Kampuni moja inayotengeneza mkate maarufu nchini Japani imetoa agizo la kurejeshwa kwa mikate elfu kadhaa na wateja kurejeshewa pesa zao baada ya mabaki ya panya kupatikana kwenye bidhaa hiyo.


Takriban pakiti 104,000 za mkate mweupe uliokatwa vipande vipande wa Shirika la Pasco Shikishima umeondolewa kwenye rafu. Sehemu za panya mweusi ziligunduliwa katika takriban mikate miwili.


Mkate wa Pasco ni chakula kikuu katika kaya nyingi za Kijapani na unapatikana kila mahali katika maduka makubwa na maduka madogo kote nchini humo.


Hakujakuwa na ripoti hadi sasa za mtu yeyote kuugua kama matokeo ya tukio hilo, Pasco ilisema katika taarifa mapema wiki hii.


“Tunaomba radhi kwa usumbufu uliojitokeza kwa wateja wetu, washirika wa kibiashara na pande zote zinazohusika,” ilisema.


Mkate huo ulitengenezwa katika kiwanda kimoja huko Tokyo, ambacho shughuli zake zimesitishwa kwa sasa.


Pasco haikueleza ni namna gani mabaki ya panya yalivyoishia kwenye bidhaa zake, lakini iliahidi “kufanya tuwezavyo kuimarisha udhibiti wetu wa ubora ili hili lisijirudie tena”.


Kampuni hiyo imechapisha fomu kwenye tovuti yake kwa wateja walioathirika kutuma maombi ya kurejeshewa pesa zao mtandaoni.


Bidhaa zake pia zinasafirishwa kwenda Marekani, Uchina, Australia, na Singapore, kati ya nchi zingine.


Agizo la kurejeshwa kwa chakula ni nadra sana nchini Japani, nchi yenye viwango vya juu vya usafi wa mazingira.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad