Maimamu ambao waliondoka nchini Morocco ili kuendesha ibada kwa Wamorocco wanaoishi Ulaya katika mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhani, wametokomea kusikojulikana na hawajarejea nyumbani hadi leo.
Taarifa kutoka Morocco zinasema Maimamu 13 waliotumwa na Wizara ya inayojihusisha na mambo Kidini kwenda nchi za Ufaransa, Ubelgiji na Ujerumani “walitoweka” wakati wakijiandaa kurejea nchini mwao.
Inaelezwa kuwa Maimamu hao wasomi wenye shahada ya kwanza, shahada ya uzamili na hata udaktari...hulipwa kila mwezi na serikali ya Morocco kwa kufanya kazi katika misikiti na hunufaika na safari ya kwenda Ulaya kuongoza sala ya mwezi mtukufu wa Ramadhani kwa gharama za serikali.
Hata hivyo, baada ya kazi yao kuisha tarehe 12 April, maimamu hao waliotumwa na Wizara ya Habbous na Masuala ya Kiislamu hawakufika kwenye uwanja wa ndege na tangu wakati huo hawajapatikana.
MCHAKATO WA UTEUZI
Safari hizi ni za kawaida kwa maimamu wa Morocco, ambayo ina mamilioni ya wahamiaji katika nchi za Ulaya.
Mchakato wa uteuzi hata hivyo ni mkali , lakini kulingana na vyombo vya habari kadhaa vya Morocco, masharti ya kupita katika uteuzi huo unatakiwa usiwe na mke wala watoto.
Kulingana na Gazeti la kila siku la Assabah, Wizara ya Habbous sasa imeamua kubadilisha masharti kwa wale watakaotaka nafasi ya kuendesha ibada nje ya nchi hususan Ulaya.
Masharti mapya itamhitaji imamu kuwa na mke na watoto kabla ya kutumwa kwenda kuendesha ibada Ulaya kipindi cha Ramadhani.