Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imesema hadi kufikia saa 3 usiku wa jana May 03,2024, Kimbunga “HIDAYA” kilikuwa katika eneo la bahari takriban kilomita 230 kutoka pwani ya Kilwa (Mkoa wa Lindi) na kilomita 170 kutoka pwani ya Mafia kikiwa na mgandamizo wa hewa wa kiasi cha 985 hPa na kasi ya upepo unaofika kilomita 120 kwa saa ambapo leo May 04,2024 kinatarajiwa kuendelea kusababisha matukio ya vipindi vya mvua kubwa na upepo mkali katika maeneo ya ukanda wa pwani hususan mikoa ya Lindi, Mtwara, Pwani na Dar es salaam pamoja na kisiwa cha Unguja na maeneo ya jirani.
TMA imesema kama ilivyotabiriwa awali, uwepo wa kimbunga “HIDAYA” karibu na pwani ya Tanzania umeendelea kutawala mifumo ya hali ya hewa kwa baadhi ya maeneo ambapo katika kipindi cha saa 12 zilizopita, vipindi vya mvua kubwa na upepo mkali vimeendelea kujitokeza, ikitolea mfano katika vituo vya hali ya hewa vya Mtwara, Kilwa, Zanzibar na Dar es Salaam ambako upepo mkali unaozidi kilomita 40 kwa saa umeweza kupimwa katika nyakati tofauti kuanzia mchana wa jana.
“Vile vile katika kipindi hicho, vipindi vya mvua kubwa vimeweza kushuhudiwa katika maeneo ya Mtwara na Lindi ambapo hadi kufikia saa 3 usiku jana kituo cha Mtwara kiliripoti milimita 61 za mvua dani ya masaa 6”
Matarajio ni kwamba kimbunga “Hidaya” kitaendelea kusogea kuelekea karibu kabisa na ukanda wa pwani ya Tanzania kuanzia usiku wa jana na mchana wa leo tarehe 04 Mei 2024 kabla ya kuanza kupungua nguvu yake kuelekea siku ya Jumapili tarehe 05 Mei 2024, siku ya leo tarehe 04 Mei 2024, kimbunga “HIDAYA” kinatarajiwa kuendelea kusababisha matukio ya vipindi vya mvua kubwa na upepo mkali katika maeneo ya ukanda wa pwani, vilevile matukio ya mawimbi makubwa baharini yanatarajiwa kuendelea kujitokeza katika ukanda wote wa mwambao wa pwani ya Bahari ya Hindi”