Maswali Matano Magumu Mwisho wa Beki Kisiki Inonga Simba

 

Maswali Matano Magumu Mwisho wa Beki Kisiki Inonga Simba

Mkataba wa beki wa Simba, Henock Inonga unamalizika mwisho wa msimu huu. Tayari ameshaitumikia Simba misimu miwili na kuonyesha kiwango bora ingawa kimekuwa kikilalamikiwa na mashabiki wa siku za karibuni.


Beki huyo wa zamani wa FC Renaissance na DC Motema Pembe za DR Congo amekuwa akihusishwa pia na timu mbalimbali zikiwamo za Afrika Kaskazini hasa za Kiarabu na tetesi zilianza tangu mwaka jana.


Kwa sasa haieleweki kama atabaki na miamba ya Msimbazi msimu ujao au ataondoka na hapa Mwanaspoti linakuletea maswali matano ambayo wengi wanajiuliza juu ya hatima yake Simba.


OFA ALIZOPATA


Ubora aliouonyesha Inonga ndani ya Simba hasa kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika na ile ya Mataifa ya Afrika (Afcon 2023) iliyofanyika Ivory Coast.


Ofa zinazotajwa ni kutoka FAR Rabat ya Morocco iliyoshindwa kumalizana naye kutokana na kuwa na mkataba wa waajiri wake wa sasa. Hata hivyo, inaelezwa kucheza chini ya kiwango ni moja ya sababu za kutaka kuondoka kwani Waarabu hao walimwekea ofa nono na atakuwa huru mkataba utakapomalizika. Swali ni je, ataziacha au atabaki?


IMANI KWA MASHABIKI


Mashabiki ni kama wamemchoka Inonga. Wamechoshwa na mwenendo wake hasa uwanjani na hawana imani naye. Wamekuwa wakimjadili mitandaoni kwa hisia hasi tangu atoke Morocco kwenye Afcon na wanaona amebadilika tofauti na alivyotu kwenye timu hiyo. Mashabiki katika mitandao ya kijamii hadi uwanjani wamekuwa wakimzonga kuonyesha kukosa imani naye kutokana na matukio ambayo amekuwa akiyaonyesha hivi karibuni, wakiweka na ushahidi wa baadhi ya matukio kuonyesha amejishusha ubora kwao.


Baadhi ya matukio hayo ni kwenye mchezo wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Tanzania Prisons ambao Simba ilichapwa mabao 2-1 na alishindwa kumaliza kwa kuumia wamanakohusisha na kutokuwa na imani na hilo.


Baada ya hapo alikosekana dhidi ya Coastal Union, Singida Fountain Gate, Mashujaa kwenye Kombe la Shirikisho (FA) na dhidi ya Yanga alicheza kwa dakika sita baada ya kutolewa kutokana na kuumia. Wanachojiuliza mashabiki ni je ataendelea kuwepo na kurudi katika kiwango chake au ndo mwisho wake Simba?


MISIMU MIWILI YA SIMBA


Inonga alijiunga na Simba kwa mkataba wa miaka miwili akitokea DC Motema Pembe ya DR Congo. Kwa kipindi chote amekuwa beki tegemeo na kama ataondoka ni wazi safu ya ulinzi itaanza upya kusukwa. Inonga alicheza sambamba na Pascal Wawa na Joash Onyango ambao walitemwa Simba kutokana na viwango vyao kushuka, lakini kipindi hicho alikuwa mwiba kwa washambuliaji wa timu pinzani na inaonekana kuondoka kwake kutaidhoofisha timu.


FAIDA NA HASARA


Kabla ya msimu huu uwepo wa Inonga kwenye safu ya ulinzi uliisaidia Simba kutoruhusu mabao hata kama timu yake haitashinda. Mashabiki walivutiwa na kiwango chake na kazi nzuri aliyofanya kabla hata ya ujio wa Che Malone.


Faida kwa Simba ni muunganiko huo na Malone aliyeingia kwenye mfumo haraka na kutengeneza pacha nzuri. Sasa mashabiki wana wasiwasi endapo ataondoka hawatapata fundi kama yeye.


Mtihani uliopo kwa Simba ni kupata mbadala wake na mwendelezo mzuri wa Inonga na Malone katika safu hiyo ni mzuri na wamecheza dakika nyingi pamoja.


KIWANGO KATIKA DABI


Msimu huu kwenye mechi za Dabi ya Kariakoo ya Yanga na Simba, mchezo wa kwanza Inonga alicheza na kushuhudia Simba ikichapwa mabao 5-1 na watani zao. Mchezo wa pili wa Ligi Kuu ulishuhudia tena Mnyama akipasuka mabao 2-1 ingawa Inonga alicheza kwa dakika sita kabla ya kuumia na kutolewa uwanjani.


Hata hivyo, kwenye michezo ya dabi tangu ajiunge na miamba hiyo amekuwa na kiwango kizuri.


Kocha Mspaniola, Pablo Franco alimpanga kwa mara ya kwanza kwenye mechi ya watani Desemba 11, 2021 na alionyesha kiwango bora akimdhibiti aliyekuwa mshambuliaji wa Yanga, Fiston Mayele mchezo uliomalizika kwa suluhu kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.


Wakati Mayele akitoka uwanjani Inonga alimsindikizwa kwa mbembe akimtambia yeye ndiye kiboko yake. Hali ikawa hivyo tena katika mechi ya marudiano ya Ligi Kuu Aprili 30, Inonga akimdhibiti ipasavyo Mayele na kumaliza mchezo bila kufunga, timu hizo zikitoka suluhu tena.


Mei 28, 2022 timu hizo zilikutana tena katika nusu fainali ya Azam Sports Federation Cup, pamoja na Inonga kumzuia Mayele kufunga, lakini Yanga ilishinda 1-0 kwa bao pekee la kiungo Feisal Salum ‘Fei Toto’ dakika ya 25 katika Uwanja wa CCM Kirumba, jijini Mwanza.


Agosti 13, 2022 katika mchezo wa Ngao ya Jamii winga Msenegali Ousmane Sakho alianza kuifungia Simba dakika ya 16 kabla ya Mayele kuisawazishia Yanga dakika ya 50 na kufunga bao la pili dakika ya 81 Uwanja wa Mkapa.


Baada ya mechi Yanga wakishangilia ushindi wa Ngao, Mayele alikwenda kumbeza Inonga wakati anaondoka uwanjani akilipa kisasi cha kufanyiwa hivyo na Mkongomani mwenzake huyo.


Kwenye mchezo wa kwanza msimu huoulimalizika kwa sare ya 1-1, Oktoba 23, 2022, Mghana Augustine Okrah akiitanguliza Simba dakika ya 15, kabla ya Mburkinabe, Stephane Aziz Ki kuisawazishia Yanga dakika ya 45. Inonga akawa na siku nzuri Aprili 16, 2023, kwani licha ya kumdhibiti Mayele asifunge bao katika mechi ya marudiano ya Ligi Kuu, lakini akafunga bao la mapema dakika ya pili la Simba kabla ya Kibu Denis kufunga la pili dakika ya 32 katika ushindi wa 2-0 Uwanja wa Benjamin Mkapa. Ilikuwa inafurahisha namna Inonga alivyokuwa akimbana Mayele asifurukute na baada ya mchezo akaenda kumtafuta kumbeza kama ilivyo ada yao.


Baada ya hapo Mayele alitimka ndani ya kikosi cha Yanga na msimu huu Inonga alikosa ubora kwani timu yake mzunguko wa kwanza ilikubali kichapo cha mabao 5-1 na mchezo wa kumaliza msimu ukiwakutanisha watani hao Simba ikaendeleza unyonge kwa kukubali kichapo cha mabao 2-1 huku yeye akicheza dakika sita.


Swali ni je ndio dakika za mwisho kucheza dabi kama inavyotajwa kuondoka au tumtarajie tena.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad