Mbunge aing’ang’ania Serikali maiti kuzuiwa kwa deni la matibabu

 


Mbunge wa Segerea, Bonah Kamoli akizungumza wakati akiuliza swali katika kikao cha 38 cha mkutano wa

Mbunge wa Segerea, Bonah Kamoli akizungumza wakati akiuliza swali katika kikao cha 38 cha mkutano wa

Suala la maiti kuzuiwa kutokana na madeni ya matibabu limeibuliwa bungeni, mbunge wa Segerea, Bonah Kamoli akieleza wabunge wamekuwa wakipigiwa simu kuombwa msaada na wananchi ambao miili ya ndugu zao imezuiwa.


Katika swali la nyongeza bungeni leo Mei 31, 2024, Bonah amehoji ni nini mkakati wa Serikali wa kuimarisha bima ya afya ili watu wapewe miili ya wapendwa wao.


“Pamoja na kauli ya Serikali bado watu katika wilaya na mikoa mbalimbali wanakutana na changamoto hiyo na sisi wabunge tunapigiwa simu kuhusu suala hili la kuzuiwa kwa maiti,” amesema.


Naibu Waziri wa Afya, Dk Godwin Mollel, akijibu swali hilo amewataka wataalamu wa afya kufuata mwongozo wa kutozuia maiti wa mwaka 2021 na wakurugenzi wa tiba washuke chini ili kufanya utekelezaji wa waraka huo.


Kuhusu bima ya afya kwa wote, amesema utaratibu utakapoanza wananchi wahamasishwe kujiunga kwa sababu ndiyo suluhisho la kumaliza tatizo hilo.


Katika swali la msingi, Bonah ametaka kujua ni ipi kauli ya Serikali kwa hospitali kutozuia maiti kwa sababu ya deni la matibabu.


Dk Mollel amesema Serikali ilishatoa maelekezo kwa vituo vyote vya kutolea huduma za afya nchini kupitia waraka namba moja wa mwaka 2021 wa kutozuia maiti.


Amesema waraka huo unataka kuweka utaratibu wa kulipia gharama za matibabu na madeni ya miili.


“Nitoe rai kwa waganga wakuu wa mikoa, waganga wakuu wa wilaya pamoja na waganga wafawidhi wa hospitali kwa ngazi zote nchini kuzingatia maelekezo ya mwongozo huu na kuhakikisha wananchi wanapata huduma pasipo kuwepo kwa vikwazo vinavyochelewesha marehemu kuzikwa,” amesema.


Serikali kwa nyakati tofauti imekuwa ikipiga marufuku uzuiaji wa maiti.


Mei 27, 2024 Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Paul Makonda alipiga marufuku hospitali mkoani humo kuzuia maiti kutokana na gharama za matibabu.


Makonda alitaka hospitali kubuni njia mbadala za kudai malipo ya gharama za matibabu.


Aliwataka wajitahidi kuwa na huruma na kuwapunguzia wananchi maumivu wanapoona hali zao ni mbaya za kifedha badala ya kuendelea kuzuia maiti.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad